Wanyama aghairi kustaafu soka ya kitaifa na kurejea Harambee Stars
BAADA ya miaka minne nje ya Harambee Stars, kiungo Victor Wanyama amebadilisha uamuzi wake wa awali wa kustaafu kutoka timu ya taifa na atashiriki mechi mbili za kirafiki nayo mwezi ujao.
Kenya inatarajiwa kucheza na Chad mnamo Juni 7 na Juni 10 kule Morocco. Kocha wa Harambee Stars Ben McCarthy Jumanne alitaja kikosi cha wanasoka 25 ambao watashiriki mechi hizo mbili.
Wanyama, 33 kiungo wa Dunfermline Athletic, alistaafu kutoka soka ya kitaifa mnamo Septemba 27, 2021. Aliamua kuchukua uamuzi huo baada ya kutimuliwa kama nahodha wa Harambee Stars na kocha wa wakati huo Jacob ‘Ghost’ Mulee ambaye alimpa jukumu hilo fowadi wa Al Duhail Michael Olunga.
Mechi ya mwisho ya Wanyama ilikuwa kwenye uwanja wa Nyayo ambapo Kenya ilitoka sare ya 1-1 na Uganda katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2022 Septemba 2, 2021.
Alikuwa amechezea Kenya mechi 60 tangu 2007 na alitajwa nahodha wa Harambee Stars mnamo 2013, akichukua nafasi hiyo kutoka Dennis Oliech.
Wakati ambapo alikuwa akistaafu, alikuwa amecheza mechi 60 kwa kuwa alichezea Stars kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 15 pekee.
Kando na Wanyama, fowadi wa FC Talanta Emmanuel Osoro pia amepata nafasi kwenye kikosi cha Stars kwa mara ya kwanza. Osoro ni wa pili kwenye orodha ya wafungaji bora katika Ligi Kuu (KPL) akiwa na magoli 16.
Wengine ambao wameitwa kikosi cha Stars kwa mara ya kwanza ni Kenneth Nyamwaya na Swale Pamba ambao wanachezea Bidco United na Bandari mtawalia.
Mechi hizo mbili za kirafiki pia zitamsaidia McCarthy kuibuka na kikosi imara cha wachezaji wanaoshiriki soka ya nyumbani ambao watawajibikia Stars kwenye Mashindano ya Soka Afrika (CHAN).
KIKOSI
KIPA
Faruk Shikhalo (Bandari FC), Sepstianos Wekesa (Kariobangi Sharks FC), Brian Bwire (Polokwane City FC)
BEKI
Siraj Mohammed (Bandari FC), Swaleh Pamba (Bandari FC), Abud Omar (Kenya Police FC), Daniel Sakari (Kenya Police FC), Lewis Bandi (AFC Leopards), Alphonce Omija (Gor Mahia FC), Kenneth Nyamwaya (Bidco United FC), Brian Mandela (Stellenbosch FC)
KIUNGO
Victor Wanyama (Dunfermline Athletic FC ), Alpha Onyango (Gor Mahia FC), Timothy Ouma (SK Slavia Prague), Brian Musa (Kenya Police FC), Ben Stanley Omondi (Gor Mahia), Boniface Muchiri (Ulinzi Stars), Mohammed Bajaber (Kenya Police FC), David Sakwa (Bandari FC), James Kinyanjui (KCB FC), Adam Wilson (The New Saints FC), William Lenkupae (Central Coastal Mariners FC)
FOWADI
Moses Shumah (Kakamega Homeboyz FC), Beja Nyamawi (Bandari FC), Emmanuel Osoro (FC Talanta)