Chebukati sasa aitaka serikali impe hela afungue seva

Na WYCLIFFE MUIA

MWENYEKITI wa Tume ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC), Bw Wafula Chebukati sasa anaitaka serikali kuipa tume hiyo pesa ili iweze kuajiri mkaguzi huru atakayetegua kitendawili kuhusu matokeo kamili yaliyokuwa kwenye sava za tume hiyo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2017.

Bw Chebukati alikiri kuwa kulikuwa na utata wakati wa kutuma matokeo ya urais hali iliyopelekea uchaguzi wa urais kufutiliwa mbali na Mahakama ya Juu na kusema IEBC sasa inasaka mkaguzi huru ili kufungua na kugakua upya mitambo ya tume hiyo.

Akiongea wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa 2017 katika jumba la mikutano la KICC, Bw Chebukati aliiomba serikali kupatia tume hiyo pesa za ukaguzi ili Wakenya wapate kujua ukweli.

“Si kweli kwamba tulikataa kufungua sava. Kile tunahitaji ni mkaguzi huru ili afungue sava na kuweka wazi kilichoendelea. Tumekosa tu pesa ili kutoa kazi hiyo kwa mkaguzi huru, na tunatumai serikali itatusaidia na fedha tulizoomba,”alisema Bw Chebukati bila kusema kiasi kamili anachotaka ili kukagua mitambo hiyo.

Bw Chebukati alimtaka mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na masuala ya Sheria, Bw William Cheptumo, aliyehudhuria uzinduzi wa ripoti hiyo, kuhakikisha IEBC imetengewa fedha za kutosha ili kutekeleza shughuli zake.

Matokeo ya urais yaliyokuwa katika sava za IEBC yaliibua utata kwani yalipelekea upinzani ulioongozwa na Raila Odinga kupinga uchaguzi wa urais na korti ikashinikiza tume hiyo kufungua sava hizo ili maafisa wa upinzani kupata matokeo hayo.

Katika ripoti yake, IEBC ilisema hakukuwa na wakati wa kutosha kufungua sava hizo kutokana na masharti makali ya usalama yaliyokuwa yameekwa kabla ya mmoja kupewa idhini ya kufungua mitambo hiyo.

Katika kesi yake ya kupinga uchaguzi, Bw Odinga alidai kuwa matokeo ya vituo 11,000 hayakuwa yanawiana na matokeo yaliyokuwa katika fomu 34A.

Bw Odinga alidai kuwa maajenti wa chama cha Jubilee walifunguliwa sava kisiri na kuvuruga matokeo ya urais yaliyowapa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto ushindi.

Hata hivyo, katika ripoti yake jana, IEBC ilichapisha orodha ya vyama vilivyopewa idhini ya kuingia kwa sava wakati kura zilikuwa zikihesabiwa.

Kulingana na IEBC, afisa wa muungano wa NASA kwa jina John Walubengo alipewa idhini ya kuingia katika sava mara 34, Davis Chirchir wa Jubilee mara 10, mgombeaji huru Collins Ndindi mara 6 naye Bildad Kagai wa Thirdway Alliance akiruhusiwa mara 5.

Bw Odinga aliwabandika washindi wa uchaguzi wa Jubilee jina ‘vifaranga wa kompyuta’ akidai hawakuchaguliwa na wapiga kura bali waliteuliwa kupitia kwa mitambo ya IEBC.

Aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduaji wa ripoti ya IEBC jana, alisema sharti tume hiyo ya uchaguzi ijikakamue ili kurejesha imani ya Wakenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Habari zinazohusiana na hii

Ruto aitetea IEBC