Nyota wa Liverpool Diogo Jota afariki katika ajali barabarani
LISBON, Ureno:
MWANASOKA nyota Diogo Jota ameaga dunia baada ya kuhusika katika ajali ya gari kaskazini mwa Uhispania akiwa na umri wa miaka 28, ripoti nchini Uhispania zimesema mnamo Alhamisi, Julai 3, 2025.
Ni wiki mbili tu baada ya Jota, 28, kufunga ndoa na mpenzi wake wa utotoni.
Inasemekana raia huyo wa Ureno alikuwa akisafiri pamoja na ndugu yake, Andre, 26, ambaye pia ni mchezaji wa soka na anahofiwa kuwa amepoteza maisha pia.
Jota alikuwa ameoa Rute Cardoso, mama wa watoto wao watatu, na katika mahojiano alitoa majuzi, alijieleza kama mwanaume mwenye bahati zaidi duniani.
Ajali hiyo ilitokea katika barabara ya A-52 katika jimbo la Zamora. Barabara hiyo ni njia muhimu inayotumiwa na madereva kutoka kaskazini mwa Ureno.
Huduma za dharura katika eneo la Castilla na Leon zimethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
“Tulipokea simu kadhaa katika kituo cha 1-1-2 Castilla y León zikieleza kuwa kulitokea ajali ya gari katika kilomita ya 65 ya barabara ya A-52, katika manispaa ya Cernadilla, Zamora. Gari liliripotiwa kuhusika katika ajali na lilikuwa likiteketea,” taarifa ilieleza.
“1-1-2 iliarifu Polisi wa Barabara wa Zamora, Kikosi cha Zimamoto cha Baraza la Jimbo la Zamora, na Kituo cha Kuratibu Dharura cha Sacyl (CCU) kuhusu ajali hiyo.
“Kutoka hapo, Kitengo cha Matibabu ya Dharura (UME) na Wahudumu wa Afya kutoka Kituo cha Afya cha Mombuey walitumwa eneo la ajali na wakathibitisha vifo vya watu wawili.”
Habari hii ya kusikitisha inakuja wiki mbili tu baada ya Jota kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Rute Cardoso, katika mji wa Porto.
-Imetafsiriwa na Geoffrey Anene