Kimataifa

Besigye azindua chama kipya cha kisiasa akiwa korokoroni

Na REUTERS July 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMPALA, UGANDA

CHAMA cha People’s Front for Freedom (PFF) kilizinduliwa jijini Kampala mnamo Jumanne huku kiongozi wake Kizza Besigye akiendelea kuzuiliwa gerezani kwa kosa la uhaini.

Wakati wa shughuli hiyo, wafuasi walibeba picha ya Besigye iliyowekwa fremu huku wakimshabikia na kulaani utawala wa Rais Yoweri Museveni kwa kumdhulumu mwanasiasa huyo “bila sababu maalum”.

Kiongozi huyo wa upinzani, alitarajiwa kuhudhuria hafla hiyo aidha kwa njia ya video au kwa kutuma taarifa isomwe kwa wafuasi wake.

Bw Besigye, ambaye amewania urais kwa mara ya nne, amekuwa kizuizini tangu Novemba mwaka jana alipokamatwa Kenya na kushtakiwa kwa kupanga njama ya kumwondoa mamlakani Rais Museveni.

Waendesha mashtaka wanadai kiongozi huyo wa upinzani alikuwa akisaka usaidizi wa kijeshi kutoka mataifa ya nje ili kuhujumu Jeshi la Ulinzi la Uganda (UDF).

Lakini mawakili na wafuasi wa Besigye wanadai mashtaka hayo yamechochewa kisiasa kwa lengo la kumzuia kuwania urais dhidi ya Museveni, 80, katika uchaguzi mkuu ujao Januari 2026.

Besigye amenyimwa dhamana mara kadhaa licha ya mawakili wake kuwasili ombi hili kwa misingi ya kuzorota kwa hali yake ya afya.

Rais Museveni aliyeingia mamlakani mnamo 1986, juzi ametangaza kuwa atawania tena urais hatua ambayo huenda ikamfanya kuandikisha rekodi ya kuwa mamlakani kwa karibu nusu karne.

Mwanasiasa chipukizi Bobi Wine pia ametangaza kuwa atakuwa debeni baada ya kupambana na Museveni katika uchaguzi uliopita wa 2021.

Haijulikani ikiwa Besigye, ambaye yuko kizuizini, atawania urais.

Mbunge Ibrahim Ssemujju, ambaye ni msemaji wa chama cha PFF, aliwaambia wanahabari Jumanne kwamba Besigye “anazuiliwa bila kufanya kosa lolote ila kwa sababu hatua hiyo kumfurahisha Museveni”.

“Nadhani wanaweza hata kuandaa karamu kusherehekea kuzuiliwa kwa Besigye,” akaeleza.

Mwanawake Museveni, Jenerali wa Muhoozi Kainerugaba, amedai kuwa Besigye alipanga kumuua babake.