Makala

Ripoti yafichua vyakula vinavyoua Wakenya kwa wingi

Na LEON LIDIGU July 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KARIBU vifo vinne kati ya kila 10 nchini Kenya sasa vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, magonjwa ya moyo na saratani — janga la kiafya linalochochewa na ulaji vyakula vilivyoongezwa sukari, chumvi na mafuta kupita kiasi.

Ripoti ya Kenya Nutrient Profile Model (KNPM) 2025 ya Wizara ya Afya inaonyesha kuwa, magonjwa haya yasiyoambukiza (NCDs) husababisha asilimia 39 ya vifo vyote, zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini, na asilimia 55 ya vifo hospitalini kote nchini.

Matokeo hayo yanaonyesha hali ya kutisha ya taifa linalokumbwa na mzozo wa lishe, ambapo angalau mtu mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 18 hadi 69 na asilimia nne ya watoto walio chini ya miaka mitano, ni wanene kupita kiasi au wanaugua unene wa kupindukia.

Wizara ya Afya inaonya kuwa, ulaji wa vyakula vyenye kalori nyingi, mafuta na sukari, pamoja na ukosefu wa mazoezi ya mwili, unahusiana moja kwa moja na ongezeko la uzani kupita kiasi na unene uliokithiri.

Katika utafiti uliofanywa kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na washirika wake, wizara ilichunguza kaunti nane — Nairobi, Machakos, Marsabit, Kajiado, Turkana, Kisii, Mombasa na Garissa — ili kuwakilisha mandhari tofauti na tabia ya ulaji nchini Kenya.

Kaunti hizi zilichaguliwa kimkakati kutokana na nafasi yao katika upatikanaji wa chakula, jiografia, mazao ya kipekee na bidhaa za thamani, pamoja na ukaribu wao na nchi jirani zinazorahisisha upatikanaji wa vyakula kutoka nje.

“Lengo kuu la utafiti lilikuwa kukusanya data kuhusu viwango vya virutubisho kwenye vyakula vinavyopakiwa vinavyopatikana nchini,” ilieleza wizara, ikisema orodha ya vyakula ililenga kukusanya taarifa za kina kuhusu lishe inayotangazwa kwenye bidhaa zinazoliwa nchini Kenya.

Wizara ilitaja lishe duni — inayojumuisha vyakula na vinywaji vyenye mafuta, sukari na chumvi kwa wingi — kama moja ya hatari kuu inayoweza kudhibitiwa kwa magonjwa yasiyoambukiza.

Utafiti huo unaonyesha jinsi mabadiliko ya tabia ya lishe pamoja na kupungua kwa mazoezi ya mwili kumechangia kuenea kwa magonjwa ya mtindo wa maisha katika makundi yote ya watu.

Janga hili linaathiri wanawake kwa kiasi kikubwa zaidi, ambapo asilimia 36.9 ya wanawake Wakenya wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wana uzito kupita kiasi na asilimia 13.4 ni wanene kupita kiasi —zaidi ya nusu ya wanawake watu wazima wakiwa na matatizo yanayohusiana na uzito.

Kwa upande mwingine, asilimia 17.3 ya wanaume ni wanene na asilimia 3.6 ni wanene kupita kiasi.

Matokeo haya yanalingana kwa karibu na ripoti ya Kenya Demographic Health Survey 2022, iliyothibitisha kuwa asilimia 45 ya wanawake na asilimia 19 ya wanaume nchini ni wanene au wana uzito kupita kiasi.

“Zaidi ya hayo, unene na uzito kupita kiasi miongoni mwa watoto na vijana wenye umri wa miaka 5 hadi 19 umeongezeka kwa kasi ya kutisha, kutoka asilimia 9.8 mnamo 2000 hadi asilimia 25.9 mnamo 2019, ambapo wasichana wameathirika zaidi,” inasema ripoti hiyo.

Mwelekeo huu unaonyesha kuwa, kwa zaidi ya miaka 19, kizazi kizima cha Wakenya kimekua kikikumbwa na mabadiliko makubwa kuhusu lishe na afya.

Katibu wa Afya ya Umma na Viwango vya Kitaaluma, Bi Mary Muthoni, alisema hali ya sasa ni ya kutisha, inayoonyesha jinsi mabadiliko ya msingi katika tabia ya ulaji yamezua janga la kiafya ambalo halijawahi kushuhudiwa.

“Kenya, kama mataifa mengine, inakumbwa na changamoto ya kuongezeka kwa magonjwa ya lishe, kutokana na mabadiliko ya mitindo ya maisha na vyakula,” alisema Bi Muthoni.

“Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari na chumvi umechangia kuenea kwa magonjwa ya moyo, kisukari na aina mbalimbali za saratani.”

Alisisitiza kuwa mabadiliko haya ya lishe pamoja na kupungua kwa mazoezi yamechangia ongezeko la unene katika kila kundi, hasa kwa vijana, wanawake na wakazi wa mijini.

Sasa imekuwa vigumu kuepuka vyakula visivyo na afya nchini. Mabango ya matangazo yako kila mahali — madukani, vituo vya magari, mabango ya barabarani — vyote vimejaa ofa za vinywaji vya soda,pizza, kuku wa kukaangwa, na vinginevyo vinavyovutia macho.

Utafiti wa Kenya STEPwise wa 2015 ulifichua tabia mbaya: Asilimia 94 ya wananchi hawali matunda na mboga kulingana na kiwango kilichopendekezwa, karibu asilimia 25 huongeza chumvi kabla au wakati wa kula, asilimia 4 hula mara kwa mara vyakula vilivyowekwa chumvi nyingi, na asilimia 84 huongeza sukari mara kwa mara wanapotengeneza vinywaji nyumbani.

Wataalamu wa afya wamebaini upungufu mkubwa wa ulinzi kwa walaji, wakisema kuwa ukosefu wa maarifa kuhusu lishe na hatari zinazotokana na ulaji kupita kiasi wa virutubishi hatari kumechangia ongezeko la maradhi yasiyo ya kuambukizwa nchini.