Habari za Kitaifa

Utajiri wa kaunti 20 waongezeka mara 3 zaidi

Na  Peter Mburu July 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Uchumi wa angalau kaunti 20 umeongezeka zaidi ya mara tatu tangu kuanzishwa kwa ugatuzi, kulingana na ripoti inayoonyesha mwenendo wa ukuaji kote nchini.

Ripoti ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO) inaonyesha kuwa kaunti hizo kwa pamoja zilikuwa na Thamani ya Jumla ya Kaunti (GCP) ya Sh1.16 trilioni mwaka 2013, ambayo ilikua hadi Sh4 trilioni kufikia 2023.

Uchambuzi wa hali ya uchumi ya kaunti uliofanywa na PBO pamoja na data kutoka Shirika la Takwimu la Kitaifa (KNBS) unaonyesha ongezeko hilo linawakilisha ukuaji wa kati ya asilimia 204 hadi 361 kwa kaunti tofauti.

Sababu kuu za ukuaji huo wa uchumi katika kaunti zimekuwa ni ufadhili kutoka kwa serikali kuu (zaidi ya Sh3.6 trilioni kwa jumla), ushuru wa ndani, uwekezaji wa serikali za kaunti pamoja na uwekezaji kutoka sekta ya kibinafsi.

Katika kipindi cha miaka 11 tangu ugatuzi uanze, karibu theluthi moja ya utajiri mpya uliopatikana nchini Kenya umetokana na kaunti hizo 20.

Kaunti tatu – Elgeyo Marakwet, Kilifi na Meru – zimeshuhudia uchumi wao ukikua zaidi ya mara nne, zikiongoza kwa ukuaji mkubwa zaidi. Kwa mfano, GCP ya Elgeyo Marakwet ilipanda kutoka Sh30.38 bilioni mwaka 2013 hadi Sh140 bilioni mwaka 2023 – ongezeko la mara 4.6. GCP ya Kilifi iliongezeka mara 4.1 hadi Sh296.4 bilioni, huku Meru ikifikia Sh484 bilioni, ongezeko la mara nne.

Kaunti hizi tatu zilipata ukuaji mkubwa, zikifuatiwa na Marsabit, Vihiga, Isiolo, Kakamega, Kwale, Bungoma, Laikipia, Bomet, Pokot Magharibi, Mombasa, Lamu, Turkana, Nyamira, Nandi, Trans Nzoia, Siaya na Mandera, ambazo zilikua mara tatu hadi 3.9.

Kitaifa, uchumi wa Kenya ulikua mara 2.8 kutoka Sh4.9 trilioni mwaka 2013 hadi Sh13.89 trilioni mwaka 2023, huku kaunti 27 zikiripoti ukuaji wa juu kuliko wastani wa kitaifa.

Takwimu za KNBS kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2023 zinaonyesha kuwa kaunti 16 ziliripoti viwango vya ukuaji vilivyo juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.6.

“Kaunti tano bora kwa ukuaji wa uchumi ni Marsabit (asilimia 9.3), Tana River (7.6), Nakuru (6.9), Kajiado (6.3), na Jiji la Nairobi (6.1),” ilisema ripoti ya GCP ya 2024 ya KNBS.

Katika kipindi hicho cha miaka 11, data inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya ukuaji ilitokea katika kaunti za Bonde la Ufa, ambako kuna kaunti sita kati ya zile 20 zilizoonyesha ukuaji wa zaidi ya mara tatu.

Ingawa haikuwa miongoni mwa kaunti zilizoongoza kwa ukuaji wa asilimia, Jiji la Nairobi lilichangia Sh2.48 trilioni (asilimia 27.7) ya utajiri mpya wa Sh8.9 trilioni uliopatikana katika kipindi hicho – mchango mkubwa zaidi kutoka kaunti yoyote.

Nairobi bado inashikilia sehemu kubwa ya uchumi wa Kenya, ikifikia asilimia 27.5 mwaka 202