Jamvi La Siasa

Pigo kwa ODM mshirika wa Raila akiunda chama

Na Wycliffe Nyaberi August 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, huenda akapata hasara kubwa kisiasa baada ya Mweka Hazina wa Kitaifa wa chama hicho Timothy Bosire, kusuka mipango ya kuondoka chamani kufuatia ushirikiano wa Raila na Rais William Ruto.

Bosire, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kitutu Masaba na mgombea wa ugavana wa Nyamira mwaka 2022, sasa anapanga kuanzisha chama kipya cha kisiasa ambacho kitatumika kama ‘silaha ya mazungumzo’ kwa niaba ya jamii ya Abagusii kuelekea uchaguzi wa 2027.

Katika mikutano iliyoandaliwa katika kijiji chake cha Nyamwanga, na hatimaye kwenye mkutano mkubwa mjini Kericho mnamo Agosti 21, 2025, wajumbe zaidi ya 700 walikubaliana kuanzisha chama kipya. Bosire alieleza kuwa tayari jina la chama hilo limetambuliwa na kuwa taratibu za usajili ziko hatua za mwisho katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP).

“Hii ni fursa muhimu kwa jamii ya Abagusii kuungana na kutoa sauti yao kitaifa. Tumezungumza na viongozi wetu waliotangaza nia ya kuwania urais kama Fred Matiang’i na David Maraga kwa lengo la kuimarisha nafasi ya jamii yetu,” alisema Bosire.

Bosire alieleza kuwa tangu kuondoka kwa Simeon Nyachae, jamii ya Kisii imekosa kiongozi wa kuiunganisha, hali aliyofananisha na kubaki “yatima kisiasa.” Aliongeza kuwa amewasiliana pia na Morara Kebaso, kijana chipukizi katika siasa, kwa lengo la kuunganisha jamii.

Hata hivyo, mpango wa Bosire umekumbana na upinzani kutoka kwa viongozi wa eneo la Kisii na Nyamira. Diwani wa Wadi ya Rigoma, Nyambega Gisesa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama kingine chenye mizizi katika jamii hiyo United Progressive Allianc e (UPA) alimtaka Bosire ajiuzulu kutoka ODM kwanza kabla ya kuendeleza mpango wa chama kipya.

“Kama kweli anamaanisha, ni vyema aondoke ODM kwanza. Hauwezi kuwa mweka hazina wa chama huku ukiunda kingine,” alisema Gisesa.

Pia alidai kuwa baadhi ya waandazi wa mkutano wa Kericho ni watu walioko ndani ya timu ya kiufundi ya makubaliano ya kisiasa kati ya ODM na UDA kuelekea 2027.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua alisema kuwa kuanzishwa kwa vyama vya kijamii kama cha Bosire kumeenea katika eneo la Gusii lakini kuna hatari ya kushindwa kuvuka mipaka ya kieneo.

“Karibu kila mwanasiasa mashuhuri wa Kisii ana chama chake. Lakini wapiga kura wa Kisii wameonyesha kuwa wako tayari kuchagua vyama au wagombea kutoka kote nchini. Hivyo basi, chama cha jamii lazima kiwe na ajenda ya kitaifa ili kivutie wafuasi zaidi,” alisema Mokua.

Aliwashauri viongozi wa jamii ya Gusii kufanya tathmini ya hali ya kisiasa ili kubaini ikiwa ni busara kuendelea na chama cha jamii au kujiunga na vyama vya kitaifa vinavyoweza kushughulikia masilahi yao.