Nitakuwa pasta nikistaafu kutoka siasa 2032 – Ruto
Na BENSON MATHEKA
NAIBU Rais Dkt William Ruto amesema kwamba analenga kazi ya kuhubiri atakapostaafu siasa katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Dkt Ruto alisema kwamba ni makosa kwa viongozi kukwamilia mamlakani kwa muda mrefu na akatangaza kuwa anapanga kuendeleza neno la Mungu baada ya kuacha siasa.
Akizungumza katika hafla ya kusherehekea miaka 50 ya kuhudumu kwa Askofu Samuel Thiong’o wa kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship of Afrika (PEFA) mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia mnamo Ijumaa, Dkt Ruto alisema kwamba alianza kazi ya kuhubiri akiwa muumini wa kanisa la African Inland Church (AIC) kabla ya kujiunga na kanisa la Pentekosti.
“Nililelewa katika kanisa la AIC lakini sasa mimi ni Mpenteskosti. Na kama alivyosema askofu (Thiongo), hii Pentekosti na Evangelisiti iko sawa na mimi kabisa,” alisema Dkt Ruto.
Kamati ya uwiano iliyoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa umma na wengi wanapendekeza Katiba irekebishwe kupunguza mamlaka ya rais.
Baadhi wamependekeza kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake na rais awe akihudumu kwa kipindi kimoja cha muda wa miaka saba pekee.
Dkt Ruto amekuwa akipinga marekebisho ya Katiba yanayolenga kubuni nyadhifa kunufaisha watu fulani.