Makala

MWOMBOLEZAJI: Heri ningekufa mimi kuliko Baba Raila Odinga


HUKU viongozi ndani na nje ya nchi wakiendelea kutuma risala za pole kwa familia, jamaa, marafiki na jamii ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, maeneo tofauti ya taifa Wakenya wameelekea barabarani kuomboleza mwanasiasa huyo shupavu.

Bw Odinga, duru zinaarifu alifariki mapema ya kuamkia Jumatano, Oktoba 15, 2025 akiwa nchini India, ambako alikuwa anapokea matibabu.

Familia ya Waziri Mkuu huyo wa zamani, pamoja na Rais William Ruto ambaye amekuwa akihudumu naye sako kwa bako tangu mwaka uliopita, hata hivyo, hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii haikuwa imetoa taarifa rasmi.

Baadhi ya wananchi wamemuomboleza Bw Odinga kwa njia ya kipekee, Homa Bay, kwa mfano wafuasi wake wakitumia ng’ombe kama nembo ya maombolezo.

Baadhi ya Wakenya wakimuomboleza Raila Odinga kaunti ya Homa Bay. Picha|George Odiwuor

Kisumu, baadhi ya maduka yamefungwa – kama ishara ya heshima kwa Bw Odinga, ambaye alitambulika kwa jina la utani kama Baba.

Bw Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu katika serikali ya mseto 2007 hadi 2012, iliyoongozwa na Rais Mwai Kibaki – ambaye kwa sasa ni marehemu.

Waziri Odinga, anakumbukwa kwa kupigania demokrasia ya Kenya haswa chini ya utawala wa Rais Daniel Arap Moi – ambaye pia ni marehemu.

Taifa Dijitali, imeandaa picha za kipekee zilizonaswa na kukusanywa na waandishi wetu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, hasa ngome ya ODM, chama alichoongoza Waziri Odinga.

Wakenya kutoka Siaya wakiwa nyumbani kwa Raila Odinga. Picha|Rushdie Ouda
Wafuasi wa Raila Odinga wakitumia ng’ombe kama nembo kumuomboleza Homa Bay. Picha|George Odiwuor
Barabara ya Jamogi Oginga Siaya, waombolezaji wakiwa wameifurika. Picha|Rushdie Ouda
Wananchi Kisii wakimuomboleza Raila Odinga. Picha|Wycliffe Nyaberi
Waombolezaji Homa Bay. Picha|George Odiwuor
Raila Odinga Stadium, Wakenya wakimuomboleza Raila Odinga. Picha|Rushdie Ouda
Maombolezo ya Raila Odinga Kaunti ya Kisumu. Picha|Rushdie Ouda