Kimataifa

Biya kuongoza Cameroon hadi afike miaka 100

Na REUTERS na CHARLES WASONGA October 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Cameroon Paul Biya, ambaye ni rais mkongwe zaidi duniani, jana alitangazwa mshindi rasmi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 12 na kupata nafasi ya kuongoza kwa muhula wa nane.

Hayo yalijiri wakati mpinzani wake mkuu, ambaye awali alijidai kushinda, alidai kulitokea milio ya risasi karibu na makazi yake.

Biya, 92, alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 53 ya kura zilizopigwa huku mpinzani wake mkuu Issa Tchiroma Bakary akipata asilimia 35.19, kulingana na matokeo yaliyotolewa jana na Baraza la Kikatiba.

Muhula mpya wa miaka saba ambao kiongozi huyo alipata utamwezesha kusalia mamlakani hadi atakapokaribia miaka 100.

Marais wengine wenye umri wa zaidi ya miaka 80 ni; Jean Lucie Sall de Tove wa Togo mwenye umri wa miaka 86, Peter Mutharika wa Malawi (85), Alassane Ouattara Ivory Coast (83) na Teodoro Obiang Nguema wa Equitoria Guinea.

Wengine ni; Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe (83), Denis Sussou Nguesso Jamhuri ya Congo (81), Yoweri Museveni wa Uganda (81) na Joseph Boakai wa Liberia mwenye umri wa miaka 80.

Kabla ya matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais kutangazwa, vikosi vya usalama vimekuwa vikikabiliana na waandamanaji baada ya matokeo ya muda kuonyesha Biya alikuwa akielekea kushinda.

Serikali haikutoa taarifa yoyote baada ya matokeo rasmi kutangazwa jana, japo wiki jana ilipuuzilia mbali madai ya upinzani kwamba uchaguzi huo ulisheheni udanganyifu.

Baada ya matokeo rasmi kutangazwa, Tchiroma aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba watu wawili waliuawa baada ya raia kushambuliwa kwa risasi nje ya makazi yake katika mji wa Garoua, kaskazini mwa Cameroon.

Hakutambua aliyefyatua risasi hizo wala kutoa kauli moja kwa moja kuhusu matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais.

Wiki iliyopita Tchiroma alidai kuwa alishinda uchaguzi na hangekubali matokeo mengine.

Kutangazwa kwa matokeo hayo kumeongeza uwezekano wa kushamiri kwa makabiliano katika ya wafuasi wa upinzani na maafisa wa usalama.

Mnamo Jumapili, watu wanne waliouawa kwenye makabiliano katika ya vikosa vya usalama na waandamanaji katika jiji la kibiashara la Douala.

“Tunatarajiwa kuwa machafuko yataongezeka huku raia wa Cameroon wakiendelea kupinga matokeo hayo rasmi. Na hatuone serikali ya Biya ikidumu kwa muda mrefu,” akasema Francois Conradie, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi katika Chuo Kikuu Oxford Economics.

“Uhalali wa ushindi wa Biya unatiliwa shaka na hivyo uongozi wa Biya hautakuwa thabiti. Raia hawaamini alishinda katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 12,” Muriithi Mutiga, Mkurugenzi wa Mipango katika Shirika la Kimataifa kuhusu Utatuzi wa Mizozo, (International Crisis Group),” akasema.

“Tunatoa wito kwa Biya kuanzisha mara moja mpango wa kitaifa wa maridhiano ili kuzuia ongezeko la fujo,” Mutiga akaongeza.

Biya, 92, aliingia mamlakani mnamo 1982 na amesalia mamlakani tangu wakati huo.

Mnamo mwaka wa 2008 aliondoa kipengele cha katiba kilichoweka idadi ya mihula ambayo rais anafaa kuhudumu. Baada ya hapo alishinda kwa urahisi.

“Biya Paul, anatawazwa kuwa Rais wa Jamhuri baada ya kupata kura nyingi zaidi,” akatangaza Rais wa Baraza la Kikatiba Clement Atangana.

Tchiroma ni msemaji wa zamani wa serikali na alihudumu kama Waziri wa Leba katika miaka ya ‘70s. Alitofautiana na Rais Biya mapema mwaka huu.