Habari

Jowi! Jowi! – Kalonzo kuzuru kaburi la Raila bila Gachagua

Na RUSHDIE OUDIA November 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Novemba 6, 2025 atatembelea kaburi la aliyekuwa Waziri Mkuu Hayati Raila Odinga kutoa heshima zake za mwisho kwa shujaa huyo.

Bw Musyoka ataandamana na kikundi cha zaidi ya watu 500 kutoka Ukambani pamoja na wafuasi wake, kuelekea Kang’o ka Jaramogi Bondo.

Kikundi hicho kitajumuisha viongozi waliochaguliwa wa Wiper, wazee wa Ukambani na wafuasi.

Kwa mujibu wa waandalizi, Musyoka atabeba ng’ombe 100 kuelekea nyumbani kwa Odinga Opoda na kuzuru kaburi lake huko Kang’o ka Jaramogi, ambapo wazee wa Ukambani wataongoza sherehe ya mazishi.

Wiki iliyopita, Musyoka alithibitisha kuwa ataongoza ziara hiyo ya kutoa rambirambi.

“Familia ya Raila Odinga ilikubali ombi letu la kutembelea Bondo, kusimama na kushiriki huzuni yao. Tunatambua kwamba kaka yetu alitaka azikwe haraka na hatukupata nafasi ya kutoa heshma za mwisho. Tumekubaliana kufanya ziara hii kuonyesha kuwa bado tuko pamoja nao,” alisema Musyoka.

Kulingana na taarifa zilizotolewa, ziara hii ni ya Wiper pekee, huku chama hicho kikikanusha ripoti zilizokuwa zikisema kuwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, angekuwa miongoni mwa watakaoambatana na Kalonzo.

Katibu Mkuu wa Wiper, Shakilla Abdallah, alisema kuwa wale watakaoambatana na Musyoka ni viongozi wa Baraza Kuu la Kitaifa  la chama chao, Magavana, Wabunge, Madiwani, wazee na viongozi wa dini.

Bi Abdallah alisema kuwa ziara hii ina umuhimu mkubwa kisiasa kutokana na historia ya ushirikiano kati ya Wiper na Orange Democratic Movement (ODM).

“Kiongozi wa chama chetu na kikundi anachoongoza wataenda tu kutoa heshima kwa kiongozi tuliyefanya kazi naye kwa karibu. Hii ni muhimu kutokana na historia ya viongozi wetu na vyama vyetu,” alisema.

Kutoka Kisumu hadi Bondo, msafara wa magari wa Musyoka unatarajiwa kuonyesha nguvu yake kisiasa katika eneo ambalo awali lilikuwa likimsaidia Odinga, rafiki yake na mshirika wa zamani katika vuguvugu mbalimbali.

Bi Abdallah alisema kuwa Musyoka na Odinga walikuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi, na uhusiano huo uliendelea hata baada ya kuwepo kwa serikali jumuishi iliyowaweka pande tofauti kisiasa.

Ziara ya Musyoka kwenye kaburi la Odinga inatarajiwa kuwa na maana kisiasa, kwani anajaribu kurithi wafuasi wa kiongozi aliyemsaidia na kusaliti matarajio yake ya urais.

Kwa Musyoka, hiki si kipindi cha maombolezo na heshima ya mwisho, bali ni onyesho la mwisho la uaminifu kwa Odinga, hata katika kifo chake, huku akiweka macho kwenye wafuasi wa ‘Raila’.

“Raila na Kalonzo walikuwa na mawasiliano kabla ya kifo cha Raila kwa sababu uaminifu wake umethibitishwa na wadau mbalimbali wa kisiasa. Ndio sababu anaonekana kuwa ndiye anayestahili kuungwa mkono na ODM na viongozi wengine,” alisema Abdallah.