• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Wafanyabiashara waililia serikali iwajengee soko la kisasa

Wafanyabiashara waililia serikali iwajengee soko la kisasa

NA RICHARD MAOSI

Wafanyibiashara katika eneo la Londiani kuelekea Muhoroni kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa iwajengee soko.

Mazingira duni ya kufanyia biashara pamoja na ukosefu wa usalama barabarani ikiwa chanzo cha hofu miongoni mwa wakazi.

Wakazi wa Londiani wanawalaumu viongozi wao kwa kuwatelekeza pindi tu walipochukua hatamu za mamlaka.

Kwa zaidi ya mwongo mmoja wamekuwa wakitoa ahadi ifikapo msimu wa kampeni za uchaguzi.

Wauzaji walioanika bidhaa zao katika njia bila kuzingatia sehemu ya kusimama magari kwa sababu ya ukosefu wa soko maalum. Picha/ Richard Maosi

Hali ni mbaya huku wauzaji wakilazimika kuendesha shughuli katika jua kali,upepo au mvua kulingana na msimu.

Pia watu wengi wamekuwa wakiugua kutokana na mkurupuko wa maradhi yanayoletwa na uchafu.

Baadhi yao wamependekeza halmashauri ya kukusanya ushuru itoze ada maalum ili waboreshewe huduma zinazozidi kudorora.

“Ni soko linalofikiwa na malori makubwa yanayoleta vitu vinavyopatikana katika masoko mengine mashinani,”Betty Chepkirui muuzaji wa viazi tamu alisema.

Malori kutoka Malaba yanavyohatarisha maisha ya wachuuzi katika barabara ya Kericho kuelekea Nakuru eneo la Londiani. Picha/Richard Maosi

Alieleza soko hili wachuuzi hufika kuanzia alfajiri,ili kuchukua bidhaa zao lakini cha kushangaza hakuna umeme.

Hali hii huwafanya wauzaji kushusha mizigo wakitumia mwangaza kutoka kwenye simu zao za mulika mwizi.

Hali hii imekuwa ikiwafanya baadhi yao kutumbukia mitaroni kando ya njia wakati wakipakia na kupakua mizigo.

Katika barabara ya Nakuru-Kericho utakumbana na wauzaji wengi,wanaotumia kila mbinu kushawishi wateja wengi wao wakiwa ni abiria na madereva wa malori ya masafa marefu.

Hatari ya kuuzia mboga karibu na barabara. Picha/Richard Maosi

Kuwania wateja katika eneo la Londiani ni jambo la kawaida hata kama itahatarisha maisha ya wachuuzi.

Wengi wao wamepoteza maisha katika mchakato wa kujitafutia mkate wa kila siku.

Baadhi ya wachuuzi hufanya kazi katika vibanda mkabala na barabara kuu,huku wengine wakiyakimbilia magari yanayosimama kuwanunulia.

Wafanyibiashara wengi hapa ni akina mama wenye umri wa makamo na vijana.Pia wachuuzi wa bidhaa rejareja wamezagaa.

Wao huuza viazi tamu,karoti, nyanya, vitunguu, viazi, kabeji na mifugo. Hekaheka ya biashara hapa husimamisha magari ya kuelekea Nairobi, Kisumu, Malaba, Kericho na Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Taifa Leo dijitali ilikita katika mzunguko wa Eldama Ravine,kushuhudia hali ilivyo.Tulibaini wauzaji walikuwa wametapakaa hadi katika sehemu za kuegesha magari.

James Korir mchuuzi wa mahindi anasema KENHA(Kenya National Highway Authority) wamepuuza majukumu yao ya kushughulikia miundo msingi.

Hawajachukua jukumu la kuweka mipaka inayoashiria barabara na sehemu ya soko.

Aidha hakuna alama za usalama zinazotumika kuwaelekeza madereva ambao ni mara ya kwanza kufika Londiani.

Sehemu ya uwanja wa mstawishaji wa kibinafsi ambayo wakazi wanaomba itengwe ili kujenga soko la kisasa. Picha/ Richard Maosi

“Kwa mfano kutoka steji ya Molo hadi Londiani,hakuna matuta hata moja njiani isipokuwa vizuizi vya polisi wa trafiki,labda ndio sababu magari mengi huenda kasi,”Korir alisema.

KENHA haijaweka vigezo vya kuzingatia,ili kuboresha uchukuzi kwa wamiliki wa magari makubwa na madogo.

Pia haijahakikisha madereva wanafuata masharti yote ya barabara kwa mujibu wa sheria za barabara(Roads Act 2007).

James anasema KENHA haijaweka mikakati ya kufanya kazi kwa ushirikiano na idara ya uchukuzi wala ofisi za umma kuratibu mijengo.

“Ili kutoa huduma bora kwa wateja muuzaji anaweza kutangaza ubora wa bidhaa kulinagana na mazingira ya kufanya biashara.”James aliongezea.

“Biashara ni nzuri katika eneo hili isipokuwa tumekuwa tukitaabika msimu wa mvua nyingi.Bidhaa zetu hunyeshewa na kuoza , tunaomba serikali ituboreshee mazingira ya kazi,”James alisema.

Aliongezea kuwa sehemu nzima ya soko haina maji safi ya kunywa,vyoo wala mapipa ya kutupia taka.

Esther Samoei muuzaji wa viazi tamu anasema,amekuwa akifanya kazi ya kuuza barabarani kwa miaka 30.

Alihamia katika sehemu ya Londiani kujiongezea idadi ya wateja kutokana na hali ngumu ya maisha mashambani.

Kundi la wanawake wanaochuuza bidhaa barabarani kwa magari ya uchukuzi na yale ya kibinafsi wakinga’ngania wateja. Picha/ Richard Maosi

Awali hakuwa akipata wanunuzi wa kutosha lakini tangu ahamie Londiani hali imebadilika kwa kujiongezea kipato maradufu.

Biashara yenyewe amemsaidia kuwasomesha wanawe wanne hadi viwango vya juu na kujinunulia kipande cha ardhi ekari mbili karibu na mji wa Molo.

“Huduma za kufanya biashara ndani ya Londiani sio za kupendeza kwanza hatuna mpangilio mzuri wa vibanda,”Esther alisema.

Pia alieleza hofu yake kuhusu visa vya ajali ambazo zimekuwa zikiripotiwa kila mara pale madereva wanapopoteza mwelekeo na kuingia ndani ya vibanda.

Miongoni mwa ajali mbaya ambazo ziliwahi kushuhudiwa katika eneo la Londiani ni ile ya Fort Ternan ambapo watu zaidi ya 50 walipoteza maisha yao 2018.

Mnamo Januari 29 mwaka wa 2019 watu wawili walipoteza maisha yao papo hapo katika ajali mbaya ya barabara ya Londiani kuelekea Muhoroni.

You can share this post!

Wanasayansi wavumbua dawa ya kuondoa usahaulifu

Mshukiwa wa mauaji ya Wakili Kimani hakuwa mgonjwa –...

adminleo