Sherehe ya mamilioni
ODM iligeuza jiji la Mombasa kitovu cha kupiga sherehe wakati wa maadhimisho ya miaka 20 huku ikitumia Sh200 milioni kufanikisha hafla hiyo ambayo pia ilitumiwa kumuenzi Kiongozi wake marehemu Raila Odinga.
Chama hicho kilianzishwa mnamo 2005 na hafla iliyoanza Ijumaa na inakamilika leo, iliwaleta pamoja viongozi, wajumbe, wafuasi na wafanyabiashara.
Mombasa iligeuzwa rangi ya chungwa huku bajeti kubwa ya chama ikihakikisha wote waliofika wanaburudika na kushiriki sherehe bila wasiwasi wowote.
Waliosafiri Mombasa walitumia treni ya kisasa ya SGR wakiketi eneo la wageni mashuhuri, walilipiwa hoteli za kifahari, mabango makubwa ya chama yakatundikwa kwenye barabara za jiji la Mombasa na kila aliyefika alipokezwa shatitao la ODM ambalo pia lilikuwa gharama kutengeza kwa sababu ya idadi kubwa ya wajumbe.
Aidha, burudani haikuachwa nyuma huku wasanii maarufu kama Majimaji wa wimbo maarufu wa Ubwogable na gwiji wa Ohangla Prince Indah Wuod Nyandare wakitumbuiza kwenye hafla ya jana iliyoongozwa na Kinara wa chama Dkt Oburu Oginga.
Mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu ODM alieleza Taifa Leo kuwa, maadhimisho hayo yamefanikiwa kutokana na mpango mahususi uliowekwa.
“Kwa wastani, sherehe hizi zimegharimu zaidi ya Sh200 milioni. Mwanzoni tuliweka mabango kote nchini, kuna kutengeneza mashatitao, bendera za chama, kuvumisha sherehe hizi kwenye vyombo vya habari, tuzo, chakula, uchukuzi na hata malazi. Kila kitu ambacho kimefanikisha sherehe hizi kinafikia pesa hizo,” akasema.
Afisa huyo hata hivyo, alisema pesa hizo zilitoka kwenye hazina ya chama na pia marafiki wakachangisha kuonyesha ukarimu wao wakati wa maadhimisho hayo.
“Siwezi kufafanua sana lakini pia tulipata pesa kutoka kwa marafiki ambao wengine sitawafichua kwa sasa,” akasema.
Uchukuzi ambao uliwashirikisha kuwabeba wajumbe hadi Mombasa ulitumia Sh50 milioni.
“Hakuna mtu ambaye hajapokea pesa ama kukwama hapa Mombasa, kila mtu alitumiwa pesa na anatumia jinsi apendavyo,” akaongeza.
Kamati ya kuratibu sherehe hiyo iliongozwa na Kiongozi wa wachache Junet Mohamed na ilijikita katika kuwalipa wajumbe, malazi na bajeti nyingine muhimu.
Mkurugenzi Mkuu wa ODM Oduor Ong’wen mnamo Ijumaa alisema ODM iliwafadhili wajumbe 3,000 kutoka maeneobunge 290 kote nchini.
Kuelekea maadhimisho hayo Alhamisi, watu 26,000 nao walikuwa wamejisajili kushiriki sherehe hizo.
“Walipewa pesa na kile wataifanyia ni maamuzi yao. Sitaki kusema ni pesa ngapi kila mjumbe alipewa kwa sababu anayetoka Kwale na mwingine Mandera hawawezi kupata pesa sawa,” akasema Bw Ong’wen.
Mahojiano na wajumbe tofauti yalionyesha kuwa waliotoka Siaya na Ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa walitumiwa Sh23,000 kugharimia chakula, usafiri na malazi.
Waliotoka Nairobi nao walipewa Sh15,000 kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ODM kaunti hiyo George Aladwa.
“Chama kilikuwa kikigharimia kila kitu na kila mjumbe amepata pesa zake. Tulikuwa na wajumbe 14 kutoka kila eneobunge la Nairobi, awali walikuwa wawe 20 lakini idadi hiyo ikapunguzwa,” akasema Bw Aladwa.
“Wajumbe kutoka Kaskazini mwa Kenya walipata hela nyingi kuliko wale wanaotoka maeneo karibu na Mombasa,” akaongeza huku akifichua kuwa ODM pia ilipata ufadhili kutoka kwa washirika wake ndani ya Serikali Jumuishi.
Ingawa hivyo, Sh200 milioni haikujumuisha pesa ambazo wafuasi ambao safari zao, malazi na chakula chao kiligharimiwa na viongozi wa kisiasa waliowasafirisha huko.
Wafuasi wa ODM nao walijaa kila mahali Mombasa huku Shirika la Reli likiongeza bogi kwenye Madaraka Express kukidhi idadi ya juu ya abiria Jumamosi.
Hata hivyo, hiyo haikutosha wengi wakiamua kusafiri kupitia mabasi na wengine ndege Ijumaa na Jumamosi.
Ndege zote zinazoenda Mombasa zilikuwa zimejaa kufikia Alhamisi na wengine waliahiri kufika Malindi na Ukunda kisha kutumia barabara hadi Mombasa.
Hoteli jijini Mombasa, Nyali, Bamburi na Diani nazo zilikuwa zimejaa kufikia Jumatano.
Sherehe zinapoisha leo, wafanyabiashara Mombasa wamebaki wakitabasamu wengine wakitaka hafla kama hizi ziwe zikiandaliwa mara kwa mara Pwani.