Serikali iwape walimu 20,000 wa JS ajira ya kudumu kwanza
MAELFU ya walimu wa shule za sekondari msingi (JS) walifanya maandamano jijini Nairobi wakiishinikiza serikali kutimiza ahadi yake ya kutoa fedha za kufadhili mpango wa kuwapa ajira ya kudumu.
Walilalamika kuwa wamehudumu kwa zaidi ya miaka miwili ilhali hawajapewa kandarasi ya kudumu.
Hii ni kinyume na msisitizo wa Rais William Ruto, kila mara, kwamba baada ya walimu hao kuhudumu kwa miaka miwili kama vibarua wanafaa kupewa ajira ya kudumu moja kwa moja.
Sasa jumla ya walimu 20,000 wa JSS ambao wamekuwa wakihudumu kama vibarua kwa miaka mitatu wameapa kususia kazi shule zitakapofunguliwa Januari endapo hawataapewa ajira ya kudumu.
Hatua hii bila shaka itavuruga shughuli za masomo katika shule za umma.
Kwa hivyo, ikizingatiwa kuwa elimu ni mojawapo ya vipaumbele vinne vikuu ambavyo serikali ya Rais Ruto inalenga kutegemea kuiwekezesha Kenya kufikia upeo wa maendeleo, serikali inafaa kusikiza kilio cha walimu hawa.
Ama kwa kweli, walimu hawa wa JS wamekuwa wakibeba mzigo mzito wa utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu wa umilisi na utendaji (CBE) kwa malipo duni; ikilinganishwa na mishahara ya wenzao walioajiri kwa mkataba wa kudumu.
Kulingana na wale ambao walikuwa wakiandamana katika barabara za jiji la Nairobi Jumatatu, wao hufundisha kwa saa nyingi lakini hulipwa Sh17,000 pekee; pesa ambazo haziwezi kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.
Aidha, walimu hawa hawana bima ya afya na hawalipwi marupurupu ya nyumba huku wale wanaofundisha katika shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum wakipitia changamoto nyingi hata zaidi.
Katika hotuba yake kwa taifa mnamo Novemba 20, 2025, Rais Ruto alitaja elimu kama mojawapo ya nyanja nne ambazo serikali inapania kuzipa kipaumbele ili kuiwezesha Kenya kujiunga na kundi la mataifa yaliyostawi zaidi duniani.
Nyanja zingine ambazo serikali inalenga kuzipa kipaumbele ni uimarishaji wa sekta za uchukuzi, kawi na uzalishaji chakula kupitia kilimo cha unyunyiziaji.
Kiongozi wa taifa aliorodhesha mafanikio ambayo serikali yake imeandikisha katika sekta ya elimu kama vile uajiri wa walimu wapya 76,000, ujenzi wa madarasa mapya katika shule za umma na kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ufadhili wa masomo ya juu.
Aidha, Dkt Ruto alitaja kwamba serikali yake imeongeza mgao wa bajeti kwa sekta ya elimu kutoka Sh490 bilioni mnamo mwaka wa 2021 hadi Sh700 bilioni mwaka huu wa kifedha wa 2025/2025. Alieleza kuwa serikali imefanya hayo, kimasudi, kwa lengo la kuhakikisha kuwa “watoto wa taifa hili wanapata elimu bora, ujuzi na ubunifu unaohitajika kustawisha jamii na taifa kwa ujumla”.
Kwa kuwa Dkt Ruto aliahidi kwamba serikali itaajiri jumla ya walimu 20,000 zaidi kuanzia Januari 2026, ingekuwa bora ikiwa wale wanaohudumu sasa kama vibarua wangepewa ajira ya kudumu kwanza.
Haina maana kwa serikali kupaza sauti kwamba itakuwa imeejiri jumla ya walimu 100,000 wapya kufikia mwaka ujao ilhali karibu 40,000 kati yao ni vibarua. Idadi hiyo ya walimu hawatakuwa wakifanya kazi kwa moyo wa kujitolea kwani kila mara watakuwa wakilalamikia hali ngumu ya maisha kutokana na mishahara duni. Katika hali kama hii, wanafunzi ndio watapoteza.