KDF yakana maafisa wake waliiba dawa za kulevya iliyonaswa Mombasa
JESHI la Ulinzi la Kenya (KDF) limekana madai kuwa wanajeshi wake walihusika katika wizi wa sehemu ya shehena ya dawa za kulevya wakati wa operesheni yao Mombasa mnamo Oktoba 25, mwaka huu.
Kwenye taarifa Jumatano, Desemba 3, 2025, KDF ilieleza kuwa kilo 1, 024 za dawa hizo aina ya ‘methamphetamine’ zilizotolewa kutoka kwa chombo fulani pwani ziko salama na zinalindwa na maafisa kutoka vitengo mbalimbali vya serikali.
“Hata hivyo, uchunguzi unaendeshwa kuhusu madai kuwa baadhi ya maafisa KDF huenda walihusika katika uovu huo. Endapo madai hayo yatathibitishwa, hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa kanuni zetu,” ikaeleza taarifa hiyo kutoka kwa kitengo cha mawasiliano cha KDF.
Mnamo Oktoba 25, 2025, kundi la maafisa kutoka asasi mbalimbali za serikali, wakiwemo maafisa kutoka KDF, walifaulu kunasa shua karibu na ufuo wa bahari likibeba kilo ya dawa ya methamphetamine.
Baadaye kuliibuka madai kuwa wakati wa operesheni hiyo, na wakati dawa hizo haramu zilikuwa zikitolewa kusafirishwa ufuoni, baadhi ya maafisa wa KDF waliohusika katika shughuli hiyo waliiba sehemu ya dawa hizo kwa matumizi yao.