Pambo

Msiruhusu sherehe za Krismasi iwe chanzo cha ugomvi

Na WINNIE ONYANDO December 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KILA mwisho wa mwaka, sherehe za Krismasi huwa zinaambatana na safari za kwenda mashambani.

Hata hivyo, kwa wanandoa wengi, kipindi hiki huleta mvutano kuhusu ni wapi watakwenda kusherehekea, watakaa kwa nani, na wanafaa kununua nini.

Wengine hukosana hadi sikukuu iishe.

Lakini haifai kuwa hivyo.

Wakijipanga vyema, wanandoa wanaweza kufurahia Krismasi kwa amani, bila kinyongo wala mvutano.

Kwanza, mawasiliano ni msingi.

Wanandoa lazima wakae chini na wazungumze kwa uwazi kuhusu matarajio yao.

Kuna wale ambao hutaka kusherehekea Krismasi kwao kila mwaka, bila kutambua mpenzi pia ana familia inayowapenda na kuhitaji kuwaona.

Mazungumzo ya mapema husaidia kupunguza mvutano kwani kila mtu anapata nafasi ya kueleza anachotaka na kwa nini.

Pili, ni muhimu kupanga mapema.

Safari za Krismasi huwa na msongamano wa magari na gharama kubwa, hivyo wanandoa wanapaswa kuanza kupanga miezi kabla ya siku yenyewe.

Hii inajumuisha kupanga usafiri, bajeti, zawadi za familia, na masuala ya malazi.

Mipangilio ya dharura huruhusu wanandoa kutulia, kuepuka ugomvi wa “mbona hukuniambia mapema,” na kufurahia sherehe.

Tatu, wanandoa wanafaa kujifunza kufanya maamuzi ya pamoja.

Kwa mfano, wanaweza kuamua mwaka mmoja kwenda kwa upande wa mume, na mwaka unaofuata kwenda kwa upande wa mke.

Aidha, wanandoa wanapokuwa mashambani, wanapaswa kujihusisha kikamilifu na shughuli za kifamilia.

Hii ni pamoja na kusaidia kupika, kufua, au kutembelea ndugu. Kujitenga au kuonekana kama mgeni haifai.

Kushiriki shughuli huimarisha uhusiano na kuvunja ile dhana ya kwamba mkwe ni mgumu.

Ni muhimu pia kupanga bajeti.

Mashambani huwa na matumizi mengi kama vile kusaidia wazee, kununua vitu vya sherehe, au kugharimia usafiri wa ghafla.

Wanandoa wanapaswa kukubaliana ni kiasi gani watatumia ili kuepuka lawama baadaye.

Bajeti ya pamoja husaidia kuweka amani na kuzuia mtu mmoja kuhisi amebebeshwa mzigo.

Mwishowe, wanandoa wanapaswa kuwa na shukrani.

Safari ya mashambani si tu kuhusu chakula na sherehe, bali inajumuisha ujenzi wa uhusiano wa kifamilia na kuunda kumbukumbu.

Ni nafasi ya watoto kukutana na ndugu zao, kujifunza tamaduni za ukoo, na kujua mizizi yao.

Kwa hivyo, badala ya Krismasi kuwa chanzo cha ugomvi, ifanyeni kuwa wakati wa kuonyesha upendo, ushirikiano na umoja.