Gachagua: Chama cha DCP hakitakubali viongozi wasio na nidhamu
KIONGOZI wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua jana alirejea Kirinyaga akiahidi wafuasi wake kwamba chama chake kitaadhibu viongozi watakaokosa nidhamu.
Alisisitiza kuwa uteuzi wa wagombeaji wa chama chake kote nchini utakuwa wa haki na huru kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Bw Gachagua alisisitiza kuwa DCP haitakuwa na wagombeaji waliopendelewa kwa viti mbalimbali vya kisiasa katika uchaguzi ujao.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Kagumo katika kaunti ya Kirinyaga ya Kati, Bw Gachagua alisema kuwa wagombeaji wa viti vya Seneti, Gavana, Wawakilishi wa Wanawake, Mbunge na Madiwani hawatapata tiketi za moja kwa moja kutoka DCP.
Aliongeza kuwa wanachama wa DCP wasiokuwa na nidhamu watafukuzwa.
“Wale wanachama wa DCP watakaotusi wapinzani wao kwenye mikutano ya kisiasa watafukuzwa kwa sababu ya kukosa nidhamu,” alisema.
Bw Gachagua alisema DCP ni chama chenye nidhamu, na wanachama watakaofanya makosa wataadhabiwa.
Aidha, alimkosoa Rais William Ruto, akidai kuwa anajitahidi kugawanya eneo la Mlima Kenya kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa.
“Rais Ruto ameamua kugawanya Mlima Kenya lakini hatutamruhusu,” alisema.
Alidai Ruto anajua kutumia watu na kisha kuwatema.
“Niliwahi kupigia debe Ruto katika Mlima Kenya na akashinda. Baada ya Ruto kuingia madarakani, alihakikisha nimefutwa kazi. Ruto ni mtu asiyeaminika, na wakazi wanapaswa kuwa makini na kukataa kugawanyika,” alisema.
Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala, aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kumchagua Gachagua na kufukuza viongozi wote wa eneo hilo wanaomkashifu.
“Viongozi wote kutoka Mlima Kenya wanaomshambulia Gachagua hawana haki ya kuongoza, wanapaswa kakataliwa,” alisema Bw Malala.
Bw Malala alimtaja Bw.Gachagua kama kigogo wa kisiasa na kumwambia Rais Ruto ajipange kwa kinyang’anyiro kikubwa kisiasa.
Aidha, Bw Malala alimkosoa vikali Rais Ruto, akisema anashughulika ‘kununua’ ODM badala ya kulipa fidia vijana wa kizazi cha Z waliouawa wakati wa maandamano dhidi ya serikali.