HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Hofu ‘Panga Boys’ wakihangaisha wakazi

Na GEORGE ODIWUOR October 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HOMA Bay imekumbwa na ukosefu wa usalama huku wakazi wakitumia majina ya utani kama vile Yemen na Haiti kurejelea hali katika kaunti hiyo.

Wakazi wanalalamikia ongezeko la kundi la magenge linalowahangaisha wafanyabiashara na wanafunzi.

Majina hayo yalianza kusambaa mitandaoni baada ya mkutano wa Linda Mwananchi uliofanyika Agosti 16, 2026, huku picha za maeneo kame ya Suba zikilinganishwa na nchi za Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, jina la Haiti lilipata umaarufu zaidi kutokana na vitisho vilivyotokana na magenge yanayodaiwa kutumia mapanga kuwashambulia na kuwaibia wananchi.

Magenge hayo yanadaiwa kuwatisha wafanyabiashara, kuwatoza madereva wa magari ya uchukuzi fedha na kuchukua chakula na vinywaji katika vibanda na mikahawa bila kulipa.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wafanyabiashara Homa Bay Jack Nyambega alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifunga maduka yao mapema kwa kuhofia kushambuliwa wanaporejea nyumbani wakiwa na mapato ya siku.

Alisema maandamano yaliyotokea baada ya kukamatwa kwa Kassim Abdi, anayezuiliwa kuhusiana na kuongoza magenge hayo, yalisababisha uporaji wa bidhaa na uharibifu wa maduka.

Bw Nyambega alisema biashara nyingi zilisitishwa, huku wafanyabiashara wadogo wakikabiliwa na changamoto za kulipa mikopo ya biashara kutokana na kukosa mapato.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tom Mboya pia wameathiriwa na hali hiyo. Mwenyekiti wa chama cha wanafunzi Collins Ouma alisema baadhi yao wameibiwa simu na pesa, huku wengine wakishambuliwa wanapotembea usiku kutafuta chakula au kushughulikia mahitaji yao.

Alitaka polisi kuongeza doria na kuwakamata wahalifu.

Katika kukabiliana na hali hiyo, polisi walianzisha operesheni kali Oktoba 10 baada ya siku mbili za maandamano yenye vurugu. Zaidi ya washukiwa 40 walikuwa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kufikia wiki iliyopita.

Polisi pia wamebomoa vibanda vinavyodaiwa kutumiwa kama maficho ya magenge hayo katika mzunguko wa Kodoyo na kituo cha mabasi. Maafisa wenye silaha wameendelea kufanya doria mjini humo.

Katibu Mkuu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo alisema operesheni hiyo itaendelea hadi amani irejee kikamilifu.

Alionya wahalifu dhidi ya kuwatisha wafanyabiashara na kuvuruga shughuli zao, akisema serikali pia itashirikiana na vijana kuwapa fursa za elimu na kujikimu kimaisha.

Kamishina wa Kaunti ya Homa Bay Ronald Mwiwawi alisema maafisa wa usalama wataendelea kulinda biashara na kuhakikisha wakazi wanaendesha shughuli zao bila hofu.