Akili MaliMakala

Anatumia malighafi ya samaki kuunda vitafunwa

Na SAMMY WAWERU October 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SAFARI ya mbali huanza kwa hatua moja, ni kauli anayoienzi Francis Thoya ambaye hutengeneza vitafunwa kwa kutumia bidhaa za kula ambazo huishia kutupwa kwa wasioona thamani yazo.

Kilichoanza kwa kuchakata kilo moja ya vitafunwa vya samaki kwa jiko dogo kimestawi na kuwa biashara inayounganisha wakulima kupitia uongezaji thamani, huku ikilenga kukabiliana na changamoto za lishe eneo la Pwani.

Kupitia EcoAfia Initiative, Thoya anasindika samaki, mihogo, moringa, njugu, korosho, nazi na mabuyu, akiunda bidhaa za kula zilivyosheheni virutubisho. Biashara iko Kilifi, ambapo inashirikiana na karibu wakulima 500 walio kwenye makundi 10, wengi wao wakiwa wanawake.

“Ni biashara changa na huzalisha kati ya kilo mbili hadi tano za vitafunwa kwa siku na hadi kilo 10 za bidhaa zilizoongezwa virutubisho,” Thoya anaiambia ‘Akilimali’. Licha ya mafanikio hayo, anasema mahitaji ya soko ni makubwa kuliko uwezo wake wa sasa wa uzalishaji.

Bidhaa za samaki

Aidha, hutengeneza aina tatu ya bidhaa—Samaki Cookie Magic Snack, Samaki Cookie Cycle Care inayolenga lishe ya wanawake, na Samaki Cookie Baby Nutrient, bidhaa iliyoongezwa virutubisho kwa minajili ya watoto. Samaki Cookie Baby Nutrient, ni unga unaotumika kuandaa uji. Kipakio cha gramu 250 ya Samaki Cookie huuza Sh50, huku Samaki Cookie Cycle Care moja ni Sh5.

Francis Thoya, mwanzilishi wa EcoAfia Initiative katika Kaunti ya Kilifi, wakati wa Mkutano wa Vijana wa Kenya kuhusu Mifumo ya Kilimo na Chakula (KYASS) 2026, uliofanyika Kenya School of Government, Kabete, Nairobi, mnamo Septemba 2, 2026. Picha|Sammy Waweru

EcoAfia Initiative ilianzishwa mwaka 2020 baada ya Kenya kukumbwa na janga la Covid-19. Thoya anasema “Nilinuwia kutumia raslimali za kilimo na baharini zinazopatikana Pwani kutengeneza bidhaa zenye thamani badala ya wakulima na wavuvi kuuza mazao na bidhaa zao kwa bei duni,” Thoya anaelezea.

Samaki Cookie, anadokeza kwamba ni kitafunwa kinachotengenezwa kwa mchanganyiko wa unga wa muhogo, unga wa samaki, moringa, njugu, korosho, nazi na mbegu za mabuyu.

“Wakulima wengi Kilifi wanajishughulisha na kilimo cha kujikimu mahitaji muhimu ya kimsingi, huku eneo hilo pia likikabiliwa na changamoto za chakula na lishe,” anasema.

Katika uchakataji wa samaki, anatumia sehemu ambazo kwa kawaida hutupwa, zikiwemo kichwa, magamba, matumbo na mifupa, ambazo hukaushwa na kusagwa kuwa unga. Unga huo huchanganywa na viungio vingine kutengeneza vitafunwa na bidhaa zilizoongezwa virutubisho, huku zikisheheni virutubisho kama vile omega-3.

Francis Thoya, mwanzilishi wa EcoAfia Initiative katika Kaunti ya Kilifi, akionyesha baadhi ya bidhaa zilizoongezwa thamani kwa kutumia samaki na mazao yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi. Picha|Sammy Waweru

Alvyoanza usindikaji

Thoya alianza biashara anayofanya kwa majaribio nyumbani kwa kutumia sufuria ndogo na hakuwa na mafunzo rasmi ya kuoka. Anasema alibadilisha mchanganyiko mara kadhaa baada ya jaribio la kwanza kuwa na harufu isiyopendeza. Baada ya miaka kadhaa ya majaribio na kupokea maoni kutoka kwa wateja, anasema alipata fomula maalum mwaka 2024.

Wahisani wamekuwa nguzo muhimu kufanikisha azma yake. “Nimepata usaidizi kutoka kwa baadhi ya wahisani na mashirika,” akasema wakati wa mahojiano.

Planet Ash ilimsaidia kupata jiko la kuoka, huku Farm Africa ikimnoa makali katika usindikaji wa samaki na uthibitishaji wa bidhaa.

Kwa sasa, changamoto kuu ni kupata vifaa vya kisasa kuongeza uzalishaji. Kifaa anachotumia, ndicho cha kukaushia samaki na kuoka vitafunwa, hivyo kupunguza kiwango cha uzalishaji. “Nikipata mashine na mitambo ya kisasa, itakuwa rahisi kuanzisha kiwanda cha uchakataji,” anaamini.

Changamoto nyingine ni athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatishia wakulima na upatikanaji wa malighafi ya kutosha. Anahimiza wakulima kukuza mazao anayohimili mikumbo ya tabianchi. Hata ingawa soko lake kuu ni Kilifi, hupata oda kutoka Nairobi, Kisumu na Nanyuki.