Shamba hili lilivyotuzwa kwa mbinuhai zake kukuza kahawa
SHAMBA la kahawa la Kiganda lenye ukubwa wa hekta 65 eneo la Gatanga, Kaunti ya Murang’a, limekuwa la kwanza Barani Afrika kupata cheti cha Rainforest Alliance Regenerative Agriculture Standard baada ya kubadili namna linavyolima kahawa kwa kuzingatia afya ya udongo, uhifadhi wa maji na mazingira.
Shamba hilo, lililokodishwa na kusimamiwa na Coffee Management Services (CMS), hutumia mbolea ya mifugo hasa samadi, mabaki ya matawi yaliyopogolewa kama matandazo, mimea inayoongeza Nitrojeni kwenye udongo na mbinu asilia kudhibiti wadudu.
Meneja Mkuu wa CMS Martin Ngare anasema Kiganda huzalisha kati ya tani 110 na 120 za kahawa mbichi kwa mwaka, sawa na karibu makontena sita, ambazo nyingi huuzwa Ulaya na Amerika. “Taji na utambuzi huu unajiri wakati mabadiliko ya tabianchi yanaathiri sekta ya kilimo, yakiweka shinikizo kwa uzalishaji wa kahawa kufuatia kuongezeka kwa kiwango cha joto, mvua isiyotabirika na kuongezeka kwa wadudu na magonjwa,” anasema.
Anasema kilimo endelevu kinasaidia kufanya shamba kustahimili changamoto hizo huku likidumisha uzalishaji na ubora. “Mjadala ni kuhusu uboreshaji wa afya ya udongo, kuhifadhi maji, kuongeza bioanuwai na kuhakikisha mazingira mazuri kwa wafanyakazi na watu wanaoishi karibu na shamba,” Ngare anaelezea.
Kiganda hufanya vipimo vya udongo ili kubaini virutubisho vinavyokosekana kabla ya kutumia mbolea. Mwaka uliopita, 2025, takriban malori 85 ya samadi yaliwekwa shambani ili kuongeza rutuba na kuboresha uwezo wa udongo kustawisha kahawa. Matawi yanayopogolewa (pruned) huachwa ardhini ili kuoza na kurejesha virutubisho.

Miti kama Albizia, Ngare anasema hutumika kutoa kivuli, kuupa udongo Nitrojeni na kusaidia kuleta virutubisho. Katika uhifadhi wa maji, udongo ulioinuliwa unazunguka mikahawa na husaidia kuelekeza maji kwenye mizizi, baada ya umwagiliaji wa juu kusababisha upotevu mkubwa wa maji wakati joto linapofikia nyuzijoto 33 hadi 35.
Udhibiti wa wadudu Kiganda Farm pia umebadilika. Badala ya kunyunyizia dawa shamba lote, wafanyakazi hufuatilia miti ili kubaini maeneo yaliyoathirika. Mbinu za kibayolojia hutumiwa pamoja na maadui wa kahawa kama vile wasps na ladybirds, huku dawa zikitumika kwa miti iliyoathirika pekee.
Julius Ng’ang’a, Mkurugenzi Mkuu wa Impact Programmes in East and Southern Africa at the Rainforest Alliance, anasema shamba la Kiganda kutambuliwa Barani Afrika ni hatua muhimu kwa sekta ya kahawa. “Hali ya hewa inabadilika, joto linaongezeka, wadudu magonjwa ya mimea yanaongezeka. Mashamba lazima yabadilike, yabadilishe mifumo yake ya uzalishaji chakula na kukumbatia ile bora na salama kwa afya ya watu,” anasisitiza.
Karugu Macharia, Mwenyekiti wa Kenya Coffee Platform, anasema kilimo endelevu si mbinu mpya. “Unapoweka samadi kwenye udongo, unaongeza rutuba na kuufanya uwe hai,” anasema, akiongeza kuwa mbinu hizo zinaweza kutumiwa hata na wakulima wadogo.

Dkt Tony Maritim, Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa, ndio Coffee Research Institute inayohudumu chini ya Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO), anasema aina za kahawa zinazostahimili athari za tabianchi kama vile ukame na wadudu zitakuwa muhimu. “Watafiti pia wanatengeneza na kutathmini aina zinazoweza kustawi katika maeneo mapya yanayolimwa kahawa,” anasema.
Kahawa inayohimili mikumbo ya tabianchi itasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji ambacho kimeshuka kwa zaidi ya asilimia 100 ikilinganishwa na miaka 30 na 40 iliyopita. Samuel Mwau, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kiufundi na Ushauri katika Coffee Board of Kenya, anadokeza kuwa uzalishaji wa kahawa nchini sasa ni karibu tani 50,000. “Uzalishaji wa kahawa kwa mkulima mdogo, ambao kihistoria ulikuwa kilo moja hadi mbili kwa mti, sasa unafikia kilo tatu na zaidi katika baadhi ya mashamba kufuatia mikahawa inayostahimili athari za tabianchi,” anasema.
Mwau anasema wakulima sasa wanapata Sh120 hadi Sh125 kwa kilo, ikilinganishwa na Sh50 hadi Sh60 miaka mitano iliyopita, hali inayochochea kurejea kwa baadhi ya wakulima katika kilimo cha kahawa.