Vyama vya kisiasa nchini sasa vimefika 107 – Msajili
VYAMA vya kisiasa vinaendelea kuongezeka nchini huku viongozi wakijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027, hali inayoibua maswali kuhusu iwapo miungano hiyo inasukumwa na sera au maslahi ya kisiasa.
Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) imetoa vyeti kamili vya usajili kwa vyama vingine sita na kufikisha jumla ya vyama vilivyosajiliwa kikamilifu 107. Zaidi ya vyama 30 vingine vina usajili wa muda, ikilinganishwa na vyama 90 vilivyokuwepo kabla ya uchaguzi wa 2022.
Wachanganuzi wanasema baadhi ya viongozi wanaanzisha au kupata umiliki wa vyama ili kudhibiti tiketi za uteuzi, kuimarisha nafasi zao katika mazungumzo ya miungano na kupata manufaa ya kifedha.
Miongoni mwa vyama vipya ni Mwongozo Mpya Party (MMP), Imarisha Uchumi Party (IUP), United Super Alliance Party (USAP), Forward Kenya Party (FKP), People’s Prosperity Party (PPP) na Freedom and Opportunity Party (FOP).
Aliyekuwa Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Eliud Owalo, aliyeanzisha PPP, amesema chama hicho kitalenga urais na pia kusimamisha wagombeaji katika nyadhifa zote za uchaguzi.
Msajili wa Vyama vya Kisiasa, John Cox Lorionokou, amevitaka vyama kuzingatia katiba zao na kuhakikisha vijana pamoja na watu wenye ulemavu wanapata nafasi sawa za kushiriki katika shughuli za kisiasa.
Vyama vingine vilivyoibuka ni Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, People’s Renaissance Movement cha Caleb Amisi na United Progressive Movement (UPM) kinachohusishwa na Boni Khalwale.
Viongozi wengine waliamua kupata umiliki wa vyama vilivyokuwapo badala ya kuanzisha vipya.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amejipatia The Equitable Party (TEP), huku Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino akijipatia Muungano Party na kukibadilisha jina kuwa Mwananchi Party (TMP).
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amepata People’s Party of Kenya (PPK), huku Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya akihusishwa na United Democratic Party.
Umiliki wa chama huwapa viongozi mamlaka ya kisheria ya kusimamia uteuzi wa wagombeaji na kuamua tiketi zitakazotolewa. Vyama pia hukusanya ada za uteuzi, ambazo zinaweza kufikia Sh50,000 kwa kila wadhifa.
Aidha, vyama vinaweza kupata fedha kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa kulingana na matokeo ya uchaguzi. Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2022 yaliongeza vyama vinavyoweza kunufaika na mgao kutoka kwa hazina hiyo.
Asilimia 70 ya fedha hizo hugawanywa kulingana na kura zilizopatikana, asilimia 15 kwa kuzingatia wawakilishi waliochaguliwa kutoka makundi maalumu, huku asilimia 10 ikitegemea idadi ya wawakilishi waliochaguliwa. Asilimia tano hutumiwa na ORPP kwa usimamizi.
Vyama pia hupata nafasi za uteuzi katika Bunge la Kitaifa, Seneti na mabunge ya kaunti.