Kaunti sasa kupokea Sh71.09 bilioni zaidi
Rais alitia saini Mswada wa Fedha za Ziada kwa Serikali za Kaunti 2026 kuwa sheria katika Ikulu ndogo ya Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, jana kabla ya maadhimisho ya Siku ya Mashujaa leo.
Fedha hizo zimeongezeka kwa Sh425.6 milioni kutoka Sh70.67 bilioni zilizotengewa kaunti katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026.
Sheria hiyo mpya pia inamtaka Waziri wa Hazina ya Kitaifa kuchapisha ripoti kila baada ya miezi mitatu kuhusu fedha zilizohamishiwa kwa serikali za kaunti. Ripoti hizo zinapaswa kutolewa ndani ya siku 30 baada ya kumalizika kwa kila robo mwaka.
Mswada huo ulidhaminiwa na Seneta Ali Roba, mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti. Ulichapishwa Machi 16, 2026, na kusomwa kwa mara ya kwanza katika Seneti Aprili 2.
Seneti iliupitisha pamoja na marekebisho Juni 17, kabla ya Bunge la Kitaifa kuupitisha pia kwa marekebisho Agosti 4. Seneti ilikubaliana na marekebisho ya Bunge la Kitaifa Oktoba 6, na hivyo kupisha mchakato wa Rais kutia saini mswada huo.
Kati ya fedha hizo, Sh56.38 bilioni ni mgao wenye masharti unaofadhiliwa kupitia mikopo na ruzuku kutoka kwa washirika wa maendeleo. Nazo Sh12.73 bilioni zitatokana na mgao wa mapato ya serikali ya kitaifa, huku Sh1.83 bilioni zikitokana na mirabaha ya madini inayostahili kaunti.