Dimba

Kombe la Dunia u17 kuanza leo rasmi

Na TOTO AREGE October 16th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KOMBE la Dunia la wanawake chini ya miaka 17, litaanza leo nchini Morocco, huku timu 24 zikitarajiwa kupigania taji hilo hadi Novemba 7.

Mabingwa watetezi Korea Kaskazini wataanza kampeni yao dhidi ya Puerto Rico, ambao wanashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza.

Mechi zingine zitakazochezwa leo ni kati ya Ujerumani na Argentina katika Kundi A, kabla ya wenyeji Morocco kukabiliana na New Zealand. Poland itamenyana na Nigeria katika mechi nyingine ya Kundi B. Mechi zote zitachezwa katika akademia ya soka ya Mohammed VI mjini Salé.

Afrika inawakilishwa na mataifa matano, yakiwemo wenyeji Morocco, Kenya, Nigeria, Zambia na Ghana.

Korea Kaskazini ndiyo timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi zaidi, ikiwa imeshinda mara nne, mwaka 2008, 2016, 2024 na 2025. Korea Kusini ilitwaa ubingwa mwaka 2010, Ufaransa mwaka 2012, Japan mwaka 2014, huku Uhispania ikishinda mwaka 2018 na 2022.

Kenya itawakilishwa na Junior Starlets, ambao wanashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya pili baada ya kucheza kwa mara ya kwanza 2024.

Kikosi hicho cha kocha Mildred Cheche kitaanza kampeni yake ya Kundi E dhidi ya China Oktoba 19, kabla ya kukabiliana na Marekani Oktoba 22 na Samoa Oktoba 25. Mechi hizo zitachezwa katika akademia ya soka ya Mohammed VI.

Cheche alitangaza kikosi cha mwisho cha wachezaji 21 jana, huku wanne wakiachwa kutoka kwa wachezaji 25 waliosafiri kwenda Morocco.

Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji walioshiriki mechi za kufuzu pamoja na chipukizi wapya, akiwemo kiungo Peninah Fostine na mshambuliaji Joan Agola, wote kutoka Shule ya Upili ya Wasichana ya Nyakach.

Mshambuliaji Mwanakombo Bakari, aliyewasili kutoka Marekani Alhamisi, pia amejiunga na kikosi hicho.

Hata hivyo, mshambuliaji Faith Boke wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere amekosa nafasi katika kikosi hicho baada ya kushindwa kupona jeraha.

Wengine walioachwa ni beki Idah Matara wa Nyakach, kiungo Clarice Demba wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Wiyeta na mshambuliaji Patience Waithira wa Shule ya Upili ya Wasichana ya St Joseph’s, Murang’a.

Kikosi cha mwisho

Walinda lango

Mishel Okoyo (Wiyeta Girls), Martha Wekhomba (Nasokol Girls), Vallary Achieng (Nyakach Girls)

Mabeki

Namisi Pauline (Desert Scorpions), Grace Mumo (Madira Girls), Bevarline Awuor (Mathare Women), Ruth Mulongo (Wiyeta Girls), Daisy Adongo (Katonje Mix), Brenda Awuor (Madira Girls Primary School), Khatenje Fleviah (St. Joseph’s, Kitale)

Viungo wa Kati

Bakari Mwanakombo (Spire Academy, USA), Beryl Okumu (Nyakach Girls), Noelina Akuku (Butere Girls), Lindey Weey Atieno (Raila School), Peninah Fostine (Nyakach Girls)

Washambuliaji

Brenda Achieng (Kakamega Hill), Elizabeth Alizeba (Oding’ Primary), Emily Adhiambo (Nyakach Girls), Wambui Tabitha (Mathare United Women), Joan Agola (Nyakach Girls), Gaudancia Maloba (Lwak Girls)