Mauaji ya Dkt Victoria Mutiso: Mumewe afichua uhasama wa kifamilia
PROFESA David Ndetei amepinga kuachiliwa kwa aliyekuwa mkewe Rose Mbithe Mulwa na watoto wao wawili, Chris na Angela, wanaoshtakiwa kwa mauaji ya mkewe, Dkt Victoria Mutiso.
Akitoa ushahidi katika Mahakama Kuu ya Milimani mbele ya Jaji Alexander Muteti, profesa huyo alisema anahofia maisha yake na ya familia yake ikiwa washukiwa hao wataachiliwa kwa dhamana.
Alidai kuwa amekuwa akitishiwa na aliyekuwa mkewe na mwanawe Chris, ambao alisema waliwahi kutishia kumnyang’anya mali yake yote na kumwacha akiwa maskini.
“Ninahofia maisha yangu kutokana na historia yangu na familia yangu ya zamani,” aliambia mahakama.
Profesa huyo, ambaye alisema hakuwa amemwona Mulwa kwa zaidi ya miaka 30 tangu aondoke nyumbani kwao Septemba 19, 1996, alikanusha madai kuwa afya yake ilimzuia kuapa na kutia saini hati ya kiapo ya kupinga dhamana.
Alisema alitia saini hati hiyo ofisini mwake Oktoba 5, 2026, mbele ya mawakili wawili.
Mulwa na watoto wake pamoja na maafisa wa polisi Elijah Kimoi na Collins Bett, Kimutai Martim na Pius Muiru wanakabiliwa na mashtaka kuhusiana na mauaji ya Mutiso Julai 29, 2026. Wote wamekanusha mashtaka.
Mahakama imeamuru ripoti za dhamana zikamilishwe ndani ya siku 14. Kesi itatajwa Novemba 4, 2026, huku washukiwa wakiendelea kuzuiliwa.