Wakenya 52 wafurushwa Amerika kwa mauaji, ubakaji na ulaghai
WAKENYA 52 wameorodheshwa katika sajili ya mamlaka ya uhamiaji ya Amerika ya watu wenye historia ya uhalifu, huku serikali ya Rais Donald Trump ikiimarisha msako dhidi ya wahamiaji.
Orodha hiyo ya Idara ya Usalama wa Ndani (DHS), inayojulikana kama Wabaya Zaidi, inajumuisha watu waliokamatwa, walio chini ya ulinzi wa uhamiaji au ambao tayari wamefurushwa kutoka Amerika.
Wakenya waliotajwa wanahusishwa na makosa mbalimbali, yakiwemo mauaji, ubakaji, unyanyasaji wa kingono, wizi wa kutumia nguvu, ulanguzi wa dawa za kulevya, kughushi hundi na ulanguzi wa fedha.
Miongoni mwao ni John Muyeka, 44, aliyekuwa akiishi Sayreville, New Jersey, ambaye alihusika katika mpango wa ulaghai uliolenga maduka katika majimbo 10 ya Amerika.
Kati ya Desemba 2013 na Februari 2017, Muyeka na washirika wake walitumia hundi za ulaghai, vitambulisho vya watu wengine na leseni bandia za udereva kupata bidhaa za thamani ya zaidi ya dola milioni mbili, sawa na takriban Sh259 milioni.
Bidhaa hizo zilijumuisha viyoyozi na mbao za sakafu za bei ya juu. Muyeka alitumia majina bandia, yakiwemo John Murunga na Daniel Okwiri, katika shughuli hizo.
Alikiri kosa la kuficha taarifa kuhusu uhalifu katika mahakama ya shirikisho mjini Newark, New Jersey, mwaka 2019, kulingana na Idara ya Haki ya Amerika.
Wakenya wengine waliotajwa ni Osbert Owuor, anayehusishwa na mauaji yaliyohusisha bunduki na kosa la kumiliki silaha, na Jackson Gichema, anayetajwa kuhusiana na ubakaji na makosa mengine ya kingono.
Bilali Wanjau Mohamed anahusishwa na ulanguzi wa dawa za kulevya na usambazaji wa kokeini, huku Collins Keanche akitajwa katika kesi ya kughushi hundi na ulanguzi wa fedha.
Adan Abdikadir anahusishwa na uvamizi wa nyumba na kushambulia, huku Winrose Ndichu akitajwa kuhusiana na ulanguzi wa fedha.
Newton Githiri, ambaye tovuti ya ICE inamtambua kama Newton Njuguna Githri, alikamatwa New Orleans Agosti 25, 2025. ICE inasema alipatikana na hatia ya kumdhulumu mtoto kingono na kuiba katika Kaunti ya Jefferson, Alabama.
Tovuti hiyo ilizinduliwa Desemba 8, 2025, kama sehemu ya kampeni ya utawala wa Trump ya kutangaza watu wenye historia za uhalifu waliokamatwa na maafisa wa uhamiaji. Kufikia Septemba 30, 2026, DHS ilisema ilikuwa na zaidi ya wasifu wa watu 40,000.
Hatua hiyo ni sehemu ya msako mpana dhidi ya wahamiaji, unaohusisha kukamatwa, kuzuiliwa na kufurushwa kwa raia wa kigeni wanaokidhi masharti ya kisheria ya kuondolewa nchini humo.
Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, Tommy Pigott, alisema zaidi ya visa 300,000 vilikuwa vimefutwa katika muhula wa pili wa Trump.
Alisema serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaokiuka sheria au kutishia usalama wa taifa.
Hata hivyo, kufutwa kwa visa na kufurushwa nchini ni hatua mbili tofauti. Kufutwa kwa visa huathiri ruhusa ya mtu kusafiri au kutafuta kuingia Amerika, huku kufurushwa kukihusisha kuondolewa kwa mtu asiye raia wa Amerika chini ya sheria za uhamiaji.
Orodha hiyo inajumuisha watu waliopatikana na hatia pamoja na wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa.