HabariHabari za Kitaifa

Mjane apinga ombi la kufukua mwili wa Saitoti kwa kipimo cha DNA

Na JOSEPH WANGUI October 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MJANE wa aliyekuwa Makamu wa Rais George Saitoti amepinga ombi la mwanamume anayedai kuwa mwana wa mwanasiasa huyo wa zamani la kufukua mabaki ya mwili wake ili kufanyiwa vipimo vya DNA kuthibitisha uhusiano wao wa damu.

Bi Margaret Wanjiku anapinga hatua hiyo akisema inaweza kusababishia wanafamilia maumivu ya kihisia, kuvuruga mahali alikozikwa mumewe na huenda isitoe sampuli zinazofaa kwa uchunguzi.

James Njage, anayedai kuwa mwana wa Saitoti, anataka mahakama ibatilishe hati ya usimamizi wa urithi, iamuru vipimo vya DNA na imtambue kama mnufaika wa mali ya marehemu.

Pia anataka kufunguliwa upya kwa kesi ya urithi ili apate maelezo ya kina kuhusu mali ya marehemu, ikiwemo mapato, matumizi, uwekezaji, akaunti za benki, kodi ya nyumba, mali iliyogawa na madeni tangu hati ya urithi ilipothibitishwa.

Saitoti, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais na Waziri wa Usalama wa Ndani, alifariki Juni 10, 2012, baada ya helikopta ya polisi aliyokuwa akisafiria kuanguka katika Msitu wa Kibiku, karibu na Ngong.

Kesi ya urithi iliwasilishwa mahakamani Nairobi mwaka huo, na tangazo likachapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali Novemba 2, 2012. Bi Wanjiku anasema hakuna pingamizi lililowasilishwa ndani ya siku 30 zilizotolewa.

Mahakama ilitoa hati ya usimamizi wa wosia Desemba 4, 2012, na kuithibitisha Januari 23, 2013. Mjane huyo anasema mali iligawanywa kulingana na matakwa yaliyoandikwa na marehemu katika wosia wake wa Februari 12, 2001.

Hata hivyo, Njage anasema hakujulishwa kuhusu kesi hiyo wala hatua za kugawa mali kwa sababu wakati huo alikuwa mdogo na hakuwa na uwezo wa kulinda maslahi yake.

“Sijawahi kushirikishwa katika kesi yoyote kuhusu usimamizi wa mali ya baba yangu, wala sijapokea taarifa, hesabu au mali yoyote kutoka urithi wake tangu alipofariki,” alisema katika stakabadhi za mahakama.

Anadai kuwa hakuna mlezi au mwakilishi wa kisheria aliyeteuliwa kumtetea, na hivyo maslahi yake kama mwana wa marehemu yalipuuzwa.

Lakini Bi Wanjiku anasema hamfahamu Njage wala madai yake ya kuwa mwana wa Saitoti.

“Sina ufahamu wowote kuhusu uhusiano anaodai kuwa nao na Saitoti, kwa hivyo siwezi kuthibitisha kuwa ni mwanawe wa kuzaa,” alisema, akiongeza kuwa Njage anapaswa kuthibitisha madai yake.

Mjane huyo pia anasema Njage hajawasilisha cheti cha kuzaliwa, kitambulisho, pasipoti au stakabadhi nyingine zinazomuunganisha na marehemu. Anadai kuwa Saitoti hakuwahi kumtambua, kumtunza au kumsaidia mwanamume huyo alipokuwa hai.

Aidha, anapinga ombi hilo akisema limewasilishwa baada ya muda mrefu kupita, akibainisha kuwa Njage amekuwa na miaka mingi ya kuwasilisha madai yake baada ya kufikisha umri wa miaka 18.

Bi Wanjiku anasisitiza kuwa hakuna udanganyifu uliofanyika katika kupata hati ya urithi wala taarifa muhimu zilizofichwa mahakamani.

Anasema mali tayari iligawiwa waliotajwa kunufaika halali na anataka mahakama kutupilia mbali ombi la Njage pamoja na gharama ya kesi.

Mali ya Saitoti ilikadiriwa kuwa na thamani ya Sh84.5 milioni mwaka 2013 kwa madhumuni ya urithi, bila kujumuisha kiasi kisichotajwa cha fedha katika akaunti tano za benki. Mali hiyo ilihusisha ardhi, nyumba, ploti magari na hisa.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Novemba 23, 2026.