Gen Z sasa walenga viti vya kisiasa 2027
VIJANA nchini wanajiandaa kuingia kwenye ulingo wa siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, huku baadhi wakisema wakati umefika wa kuacha kupinga sheria kwa kuandamana barabarani na kuingia bungeni kuzitunga.
Utafiti uliofanywa na shirika la Youth Congress umebaini kuwa vijana 113 wanapanga kuwania nyadhifa za uchaguzi, wengi wakilenga viti vya wawakilishi wa wadi (MCA).
Kati yao, 74 wanataka kuwa MCA, 21 wanalenga ubunge, saba wanataka viti vya wawakilishi wa wanawake, sita wanawania useneta na mmoja anataka ugavana. Hakukuwa na kijana aliyetangaza nia ya kuwania urais wakati wa utafiti huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Youth Congress Raphael Obonyo alisema utafiti huo ulifanywa kati ya Juni 1 na Julai 31, 2026, kubaini idadi ya vijana wanaotaka kuwania, nyadhifa wanazolenga na sababu zinazowasukuma kujiunga na siasa.
Alisema wengi wamechoshwa na huduma duni, ukosefu wa ajira na changamoto za maji, usafi wa mazingira, afya na kilimo.
“Baadhi yao walisema wanajiunga na siasa kutokana kwa kutamaushwa na uongozi uliopo,” alisema Obonyo.
Vijana wengine wanaamini wanaelewa changamoto za kizazi chao na wanaweza kuzishughulikia wakiwa viongozi.
Usimamizi wa taka ni mojawapo ya masuala wanayotaka kupewa kipaumbele. Obonyo alisema vijana katika kaunti za Nairobi, Kakamega, Nakuru, Kisumu, Kiambu na Mombasa wanataka kushirikishwa rasmi katika ukusanyaji taka na uhifadhi wa mazingira, shughuli ambazo baadhi yao tayari huzifanya kujipatia riziki.
Wengine wanataka serikali zitambue fursa zilizopo katika teknolojia, michezo na sekta bunifu, huku wakilalamikia ukosefu wa intaneti katika maeneo ya mashambani.
Kulingana na Obonyo, gharama ndogo ya kampeni za MCA inaweza kuwa sababu ya vijana wengi kulenga viti hivyo, huku wengine wakivitazama kama njia ya kupata uzoefu kabla ya kuwania nyadhifa za juu.
Wanawake walikuwa asilimia 15 ya waliohojiwa, ikilinganishwa na wanaume waliokuwa asilimia 85. Obonyo alisema vijana wa kike hukumbana na ukatili mtandaoni na nje ya mtandao, ukosefu wa fedha za kampeni na mitazamo inayowabagua.
Baadhi yao wanataka kupigania upatikanaji wa sodo za hedhi, suala ambalo wanasema wanasiasa hulizungumzia wakati wa kampeni lakini wanalisahau baada ya uchaguzi.
Maandamano yaliyoongozwa na Gen Z mwaka 2024 kupinga Mswada wa Fedha yaliwahamasisha vijana wengi kushiriki siasa. Hata hivyo, baadhi sasa wanasema maandamano pekee hayawezi kuleta mageuzi wanayotaka.
Meshack Kiprotich, mwenye umri wa miaka 23 na katibu wa masuala ya vijana wa KANU, alisema alishiriki maandamano Nairobi kabla ya kurejea Kericho kuhamasisha vijana.
“Tunahitaji vijana wawe watunga sheria. Hatupaswi kuwa nje kila mara tukipinga sheria. Tunapaswa pia kuwa ndani ya Bunge tukitunga sheria bora,” alisema.
Takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zinaonyesha wapiga kura wenye umri wa miaka 18 hadi 35 walikuwa asilimia 51 ya waliosajiliwa mwaka 2017, lakini idadi hiyo ilishuka hadi asilimia 39.84 mwaka 2022.
Mwaka 2017, vijana 3,428 waliwania nyadhifa mbalimbali, lakini 314 pekee walishinda. Kati yao, 287 walikuwa madiwani, 17 wabunge, sita maseneta, watatu wawakilishi wa wanawake na mmoja gavana.
Allans Ademba wa mpango wa “Tuko Kadi” alisema idadi ya wapiga kura waliosajiliwa kupitia kampeni hiyo iliongezeka kutoka 2.6 milioni hadi 2.9 milioni kufikia Agosti 2026.
Anataka idadi hiyo ifikie milioni sita na vijana washinde angalau viti 100 vya uchaguzi.
“Mpiga kura aliyesajiliwa ana nafasi nzuri zaidi ya kuleta mabadiliko kuliko mwandamanaji ambaye hajajisajili,” alisema.
Hata hivyo, vijana wengi bado hawajaamua vyama watakavyotumia, huku wengine wakipanga kuwania kama wagombea huru.