Waititu apata pigo tena akipoteza kesi
ALIYEKUWA gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kukataa kufuta sheria inayowazuia waliopatikana na hatia ya ufisadi kushikilia nyadhifa za umma kwa miaka 10.
Jaji Enock Chacha Mwita alisema Waititu na walalamishi wengine walishindwa kuthibitisha kwa nini Kifungu cha 64 cha Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi kinapaswa kutangazwa kuwa kinyume cha Katiba.
Sheria hiyo inawazuia waliopatikana na hatia ya ufisadi au uhalifu wa kiuchumi kuchaguliwa au kuteuliwa katika nyadhifa za umma kwa miaka 10 baada ya kuhukumiwa.
Waititu anatumikia kifungo cha miaka 12 kuhusiana na sakata ya ufisadi ya Sh588 milioni iliyohusisha utoaji wa zabuni ya ujenzi wa barabara Kiambu kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited.
Alitozwa faini ya Sh53.5 milioni au kifungo cha miaka 12 gerezani. Aliyekuwa afisa mkuu wa barabara Kiambu Luka Mwangi Wahinya alitozwa Sh21 milioni au kifungo cha miaka saba, huku mkurugenzi wa kampuni hiyo Charles Chege Mbuthia akitozwa Sh295 milioni au kifungo cha miaka tisa.
Walalamishi walipinga vifungo hivyo, wakisema vilizidi viwango vilivyowekwa na Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Hata hivyo, Jaji Mwita alisema mahakama ya rufaa ndiyo iliyofaa kushughulikia masuala hayo.
“Mamlaka ya mahakama hii si mbadala wa mamlaka ya mahakama ya rufaa,” alisema.
Rufaa zao dhidi ya hukumu na adhabu zilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu inayoshughulikia kesi za ufisadi.
Waititu, mkewe Susan Wangari na washirika wao wanatarajiwa kufika mahakamani Oktoba 27, 2026, kwa hatua ya kupunguziwa adhabu na kuhukumiwa kuhusu makosa ya kufua fedha na kupokea mapato ya uhalifu.