Sababu za maelfu ya walimu kufeli mtihani wa Diploma
KUPUNGUZWA kwa alama za kujiunga na mafunzo ya diploma katika ualimu wanaofunza shule za msingi kumetajwa kuwa mojawapo wa sababu za idadi kubwa ya wanafunzi kufeli mtihani wa mwaka huu.
Matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) yanaonyesha kuwa watahiniwa 9,792 kati ya 25,098 waliofanya mtihani, sawa na asilimia 39.02, watarudia baadhi ya masomo kabla ya kuhitimu.
Hisabati ndiyo iliyokuwa na changamoto kubwa zaidi, huku watahiniwa 6,815 wakifeli somo hilo. Kiswahili kilikuwa na 2,988 waliofeli, huku Kiingereza kikiwa na 1,514.
Hili ndilo kundi la kwanza kufanya mtihani tangu masharti ya kujiunga na vyuo vya ualimu yapunguzwe kutoka alama ya C katika KCSE na mahitaji maalumu katika masomo kadhaa.
Mkurugenzi mkuu wa KNEC, Dkt David Njengere, alisema kuondolewa kwa sharti la kupata alama ya C katika Hisabati na Kiingereza kuliruhusu wanafunzi wenye alama za chini kujiunga na masomo hayo.
“Changamoto kubwa ni uwezo wa wanafunzi wanapojiunga. Sharti la kupata C liliondolewa kwa sababu wanafunzi waliokuwa wakifuzu kuingia vyuo vya diploma walikuwa wachache,” alisema.
Kati ya watahiniwa wa mwaka huu, ni 3,644 pekee waliokuwa na alama ya C au zaidi katika Hisabati ya KCSE, huku 17,137 wakiwa na alama kati ya D na E.
Dkt Njengere alisema sababu nyingine zinazoweza kuchangia matokeo hayo ni ongezeko la wanafunzi, uhaba wa walimu wa vyuo, vifaa duni na changamoto za kutekeleza tathmini ya wanafunzi wanapokuwa masomoni.
KNEC inapanga kufanya mtihani Januari 2027 kwa watahiniwa ambao hawakufikia kiwango kinachohitajika kuhitimu.
Naibu katibu mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Hesbon Otieno, alisema matokeo hayo yanahitaji uchunguzi kubaini kama wakufunzi wana ujuzi wa kutosha kufundisha kulingana na mtaala unaozingatia umilisi.
Alisema vyuo vinahitaji vifaa vinavyowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo badala ya kutegemea nadharia pekee.
Chuo cha Mosoriot kilirekodi idadi kubwa zaidi ya waliorejeshwa, kikiwa na watahiniwa 927 kati ya 964. Nakuru kilikuwa na 541 kati ya 548, huku Borabu kikiwa na 538 kati ya 627.
Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi, Silas Obuhatsa, alitaka Wizara ya Elimu kuchunguza matokeo hayo, akitaja changamoto za karo, miundombinu na nidhamu miongoni mwa wanafunzi kama mambo yanayoweza kuchangia.
Alisema hatua za haraka zinahitajika kusaidia watahiniwa walioathirika na kuboresha ubora wa mafunzo ya walimu.