Habari za Kitaifa

Watu saba hawajulikani waliko baada ya jengo kuporomoka Eastleigh

Na HILLARY KIMUYU, BENSON MATHEKA October 24th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Watu saba bado hawajulikani waliko baada ya jengo la ghorofa 18 kuporomoka Eastleigh, Nairobi, huku shughuli za uokoaji zikiendelea kwa tahadhari kutokana na hofu ya kuathiri hewa inayoweza kuwasaidia manusura walio chini ya vifusi.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alisema wafanyakazi 67 waliokuwa wakijenga jengo hilo kando ya 9th Street kabla ya kuporomoka wamepatikana. Mmoja alijeruhiwa huku wengine 66 wakinusurika bila majeraha.

Hata hivyo, watu saba wanaoaminika kuwa walikuwa katika maduka 11 kwenye ghorofa ya chini na sehemu ya chini ya jengo hilo hawakuwa wamepatikana kufikia Ijumaa jioni.

“Tuna matumaini kuwa wako salama na shughuli hizi za uokoaji zitahakikisha wanaokolewa wakiwa hai,” alisema Bw Murkomen.

Shughuli za uokoaji ziliendelea hadi usiku, lakini zilikumbwa na changamoto baada ya kuripotiwa kuwa watu waliokuwa chini ya vifusi walilalamika kuwa mashine za kuchimba zilikuwa zikiathiri upatikanaji wa oksijeni.

Waokoaji walisitisha kwa muda matumizi ya mashine hizo ili kushauriana kuhusu njia salama ya kufikia watu hao bila kuhatarisha maisha yao.

Bw Murkomen alisema eneo hilo lilihitaji utaalamu wa wahandisi ili kuondoa vifusi bila kusababisha janga zaidi.

Timu ya pamoja inayojumuisha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), polisi, serikali ya kaunti ya Nairobi, Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya inaongoza shughuli hizo.

Wakati huohuo, Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) imetaja kampuni na wataalamu walioorodheshwa katika rekodi zake kuhusu mradi huo.

Mamlaka hiyo ilisema kampuni ya 9th Street Plaza Limited ndiyo msanidi wa jengo hilo, huku Stromax Holdings E.A Limited ikiwa mkandarasi. Rekodi hizo pia zinamtaja Emmanuel Mwangi Maina kama mbunifu na Joseph Muturi Mugu kama mhandisi wa miundo.

NCA ilisema mradi huo ulisajiliwa Julai 30, 2025. Hata hivyo, taarifa hiyo haikubainisha ikiwa jengo hilo lilikaguliwa kabla ya kuporomoka au kama kulikuwa na ukiukaji wa usalama uliokuwa umeripotiwa.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alisema jengo hilo halikuwa na cheti cha kuruhusu watu kuanza kulitumia.

Chanzo cha kuporomoka kwake bado hakijabainika, huku uchunguzi ukitarajiwa kubaini iwapo kulikuwa na uzembe au ukiukaji wa kanuni za ujenzi.

Bw Murkomen alionya kuwa wahandisi, wasimamizi wa ujenzi na wataalamu wengine watakaopatikana kuhusika na uzembe wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu.

“Njia za mkato hazitatusaidia kama nchi. Ufisadi hautatusaidia. Kutafuta pesa za haraka kunaweza kugharimu maisha,” alisema.

Aliwataka maafisa wa serikali za kitaifa na kaunti kukagua majengo nchini ili kuhakikisha yanazingatia viwango vya usalama.

Waziri huyo alisema tukio la Eastleigh ni la pili la kuporomoka kwa jengo kuripotiwa Nairobi mwaka huu, akitaka wanaohusika na ukiukaji wa sheria wawajibishwe.

Kwa sasa, kipaumbele cha mamlaka ni kuwatafuta watu saba ambao hawajapatikana, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha mkasa huo na iwapo kuna mtu au taasisi iliyoshindwa kutekeleza wajibu wake.