Habari

Onyo kali kwa wanaotumia akaunti za M-Pesa za wengine kulangua pesa

Na NDUBI MOTURI October 24th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amewaonya Wakenya dhidi ya kuruhusu watu wengine kutumia akaunti zao za benki, laini za M-Pesa na vitambulisho kuhamisha pesa zinazotiliwa shaka, akisema wanaweza kujipata wakichunguzwa kwa uhalifu.
Bw Ingonga alisema vijana wako katika hatari zaidi ya kutumiwa na mitandao ya wahalifu kufanikisha ulanguzi wa pesa na uhalifu mwingine wa kifedha.
“Msiruhusu akaunti zenu za kifedha, vitambulisho au majukwaa ya kidijitali kutumiwa kwa shughuli za uhalifu,” alisema wakati wa mkutano wa mazungumzo na wananchi katika Kanisa la AIC, Riruta, Nairobi.
Alisema baadhi ya watu huruhusu marafiki na jamaa kutumia akaunti zao bila kujua chanzo cha pesa zinazopitishwa humo. Alionya kuwa wanaosaidia kuhamisha pesa haramu wanaweza kuwajibishwa kisheria kulingana na ushahidi.
Bw Ingonga alikuwa akizungumza katika hafla hiyo kupitia mpango wa Ofisi ya DPP wa Chapa Gumzo na Prosecutor, unaolenga kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu mfumo wa haki za jinai.
Pia alionya dhidi ya ulaghai mtandaoni, vitisho vya kidijitali na matumizi mabaya ya Akili Unde kuunda picha, video na sauti bandia.

Aliwahimiza vijana kulinda taarifa zao binafsi wanapotumia mitandao, huku akisisitiza kuwa vita dhidi ya uhalifu wa mtandaoni lazima viheshimu haki za kikatiba, zikiwemo faragha na uhuru wa kujieleza.

Kamishna wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, Jerusah Mwaathime, aliwataka vijana kukataa kujiunga na magenge ya uhalifu na kuepuka kusambaza maudhui yanayochochea vurugu.
Onyo hilo linajiri huku ripoti ya Kituo cha Kuripoti Uhalifu wa Kifedha (FRC) ya mwaka 2024 ikionyesha kuwa kilichanganua ripoti 9,571 za shughuli zinazotiliwa shaka.
Mamlaka zinaonya kuwa wahalifu hutumia akaunti za watu wengine kuficha chanzo cha pesa.
Wakenya wanashauriwa kutokubali kuhamisha pesa wasizojua zilikotoka, kulinda siri zao za M-Pesa na kutotoa taarifa binafsi kwa watu wanaowapigia simu wakijifanya maafisa wa kampuni za huduma za kifedha.