Watu wahofiwa kukwama baada ya jengo la ghorofa 18 kuporomoka Eastleigh Nairobi
WATU kadhaa wanahofiwa kukwama chini ya vifusi baada ya jengo la ghorofa 18 kuporomoka katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi, Ijumaa.
Jengo hilo lilikuwa kwenye Barabara ya Yusuf Haji, karibu na duka la Day to Day kwenye 9th Street, eneo lenye shughuli nyingi za biashara.
Timu za uokoaji kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya na serikali ya kaunti ya Nairobi zilitumwa eneo hilo kusaidia kuwaokoa watu waliokuwa chini ya vifusi.
Mkuu wa Polisi eneo la Nairobi, Issa Mohamed, alisema shughuli za uokoaji zilikuwa zikiendelea huku maafisa wa polisi wakijaribu kudhibiti umati wa watu waliokuwa wamefurika eneo la tukio.
Polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya watu waliokuwa wakifunga njia za kuingia eneo la tukio kurahisisha kazi ya waokoaji.
“Wahudumu wa dharura wako eneo hilo huku juhudi zikiendelea kutafuta manusura,” alisema Bw Mohamed.
Aliongeza kuwa maafisa zaidi wa polisi walitumwa kusaidia kuratibu shughuli za uokoaji na kuhakikisha magari ya dharura yanafika eneo hilo bila vikwazo.
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, aliyetembelea eneo la tukio, alisema kipaumbele cha serikali ya kaunti ni kuokoa maisha ya watu waliokuwa wamekwama chini ya vifusi.
Alisema mashine za kuchimba vifusi, vifaa vya kuvunja simiti na mbwa maalumu wa kutafuta watu zilitumwa kusaidia shughuli hizo.
“Lengo letu kwa sasa ni kuokoa maisha. Tunaondoa vifusi na kuunda nafasi ili hewa ya oksijeni iwafikie watu wanaowasiliana nasi kutoka ndani ya jengo,” alisema.
Bw Issa alisema mtu mmoja aliokolewa kutoka vifusi na kupelekwa hospitalini. Alisema mtu huyo alikuwa katika hali nzuri.
Jengo hilo lilikuwa bado linajengwa lilipoporomoka, ingawa ghorofa za chini zilikuwa tayari zikitumiwa na wafanyabiashara na wapangaji.
Mmoja wa wafanyakazi walionusurika, Alexander Kidida, alisema wafanyakazi waligundua nyufa kwenye nguzo moja na kuamua kutoka nje mbio.
“Tuliona nguzo moja ilikuwa na nyufa, kwa hivyo tukaamua kukimbia kujiokoa. Dakika chache baadaye, jengo liliporomoka,” alisema.
Alikadiria kuwa takriban watu 70 walikuwa wakifanya kazi katika jengo hilo, lakini hawakuwa wamehesabu ni wangapi waliofanikiwa kutoka salama.
Alisema baadhi ya wafanyakazi wenzake walikuwa kwenye sehemu ya chini ya jengo na hawakuwa wamepatikana.
Joseph Kaula, aliyekuwa akifanya kazi kwenye ghorofa ya tano, alisema alisikia watu wakipiga mayowe nje na baadaye akahisi jengo likitikisika.
“Nilidhani watu walikuwa wakipigana nje. Nilipoanza kutoka, nilisikia jengo likitikisika na nikaruka. Nilikuwa miongoni mwa watu wa mwisho kutoka. Mungu ni mkuu,” alisema.
Jacob Obiero aliyeshuhudia mkasa huo alisema marafiki zake wawili waliokuwa wakifanya kazi ndani ya jengo hilo hawakuwa wamepatikana, huku simu zao zikiwa hazipatikani.
Baadhi ya mashahidi walisema huenda idadi ya watu waliokuwa ndani ilikuwa ndogo kwa sababu tukio hilo lilitokea wakati wa sala ya adhuhuri, ambapo wafanyabiashara wengi walikuwa wamefunga maduka yao kwenda kusali.
Bw Sakaja alisema jengo hilo halikuzingatia kanuni za ujenzi na akaahidi hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya anayelimiliki.
Hadi wakati wa taarifa ya awali ya kaunti, idadi kamili ya watu waliokuwa wamekwama, majeruhi na chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo havikuwa vimebainika.