Habari

Utata kuhusu hatua ya wabunge kuzima matangazo ya moja kwa moja ya matokeo ya uchaguzi 2027

Na SAMWEL OWINO October 24th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

UAMUZI wa wabunge kukataa marekebisho yaliyopendekezwa na Seneti na Mbunge wa Suba South Caroli Omondi kuhusu matangazo ya moja kwa moja ya matokeo ya urais umeibua utata kuhusu uwazi wa uchaguzi nchini.
Bunge la Kitaifa lilipitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa 2024 Alhamisi, licha ya upinzani kutoka kwa baadhi ya wabunge waliotaka kuwe na utaratibu wa kutangaza matokeo yanapohesabiwa katika maeneo bunge.
Bw Omondi alipendekeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iwe na mfumo wa kutangaza moja kwa moja matokeo yaliyotangazwa katika vituo vya kuhesabia kura, ikiwemo kura za Wakenya wanaoishi ughaibuni.
Hata hivyo, Bunge lilikataa mapendekezo hayo, likisema marekebisho hayo yalikuwa yakilenga kifungu ambacho tayari kilikuwa kimefutwa katika mswada huo.
Hatua hiyo imeibua wasiwasi kwa sababu kifungu cha 39(1G) cha Sheria ya Uchaguzi, kinachotaja matangazo ya moja kwa moja kuwa kwa ajili ya kuwafahamisha wananchi pekee, kilikuwa kimetangazwa kinyume cha Katiba na Mahakama Kuu.
Mahakama ilipinga kifungu hicho kwa kudhoofisha hadhi ya matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura.
 Hata hivyo, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah alisema Bunge halijapiga marufuku matangazo hayo na kwamba kifungu hicho bado kinatumika.
Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alionya kuwa kufuta mapendekezo hayo kunaweza kuibua tena wasiwasi kuhusu uwazi na ucheleweshaji wa kutangaza matokeo.
Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed pia alionya dhidi ya kubadilisha sheria za uchaguzi muda mfupi kabla ya uchaguzi, akirejelea mapendekezo ya ripoti ya Kriegler.
Mswada huo sasa utarejeshwa kwa Seneti kwa mujibu wa Katiba.
Katika marekebisho mengine, wabunge walitaka IEBC kuwasilisha sajili zilizokaguliwa kwa Bunge la Kitaifa na Seneti, huku wakipitisha masharti kuhusu ushahidi wa kidijitali katika kesi za uchaguzi.