Mutua kulipa Nonini fidia ya Sh3 milioni kwa kumchafulia jina
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Music Copyright Society of Kenya (MCSK) Ezekiel Mutua ameamriwa kumlipa mwanamuziki Nonini fidia ya Sh3 milioni kwa kumchafulia jina kupitia mitandao ya kijamii.
Hakimu James Gitau alimwamuru Mutua kumlipa Nonini ambaye majina yake halisi ni Hubert Nakitare, Sh2.5 milioni kama fidia ya kawaida na Sh500,000 kama adhabu ya ziada kutokana na matamshi aliyotoa dhidi yake.
Mutua pia ameamriwa kuondoa machapisho hayo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Mzozo huo ulianza Januari 2024, MCSK ilipotangaza kuwa ingesambaza Sh20 milioni za mirahaba kwa wanachama wake 1,600.
Nonini, ambaye alikuwa ameondoka katika MCSK Mei 2022, alihoji kiasi hicho baada ya kupata stakabadhi alizoamini zilionyesha kuwa shirika hilo lilikuwa limekusanya mamilioni zaidi ya lililotangazwa.
Alisema MCSK ilikuwa imekusanya Sh109 milioni kutokana na mirahaba kati ya Januari na Desemba 2023, huku Sh57 milioni zikitumika kulipa mishahara ya wafanyakazi.
Mwanamuziki huyo, anayejulikana kama Godfather wa Genge, alichapisha madai yake mtandaoni akitaka uwazi kuhusu jinsi fedha za wanamuziki zilivyokuwa zikisimamiwa.
Hata hivyo, mjadala huo uligeuka kuwa mzozo binafsi baada ya Mutua kumtaja Nonini kuwa mkimbizi wa sheria na kumshutumu kwa kufuja fedha za wanamuziki alipokuwa akihudumu katika mashirika mengine ya hakimiliki.
Mutua pia alidai kuwa Nonini alikuwa amesambaza stakabadhi bandia kuhusu hesabu za MCSK na kusema suala hilo lilikuwa limeripotiwa kwa polisi.
Nonini aliambia mahakama kuwa madai hayo yalimsawiri kama mhalifu aliyekimbilia Amerika kukwepa mkono wa sheria, hivyo kuharibu sifa yake. Alisema Mutua pia alirudia madai hayo katika mahojiano na kituo cha redio cha Hot 96.
Hakimu alisema matamshi hayo yalikuwa na uwezo wa kuharibu sifa ya Nonini kwa kumsawiri kama mtu anayekwepa sheria.
Hukumu hiyo ni pigo jingine kwa Mutua, ambaye pia anakabiliwa na kesi ambayo Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), inataka arejeshe Sh27 milioni. Tume hiyo inadai alipandisha mshahara wake na kujilipa marupurupu kinyume cha sheria alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Film Classification Board (KFCB).