HabariHabari za Kitaifa

Ruto awarai wawekezaji wa Urusi na miradi ya Sh5.2 trilioni Kenya

Na MERCY SIMIYU October 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amewaalika wawekezaji wa Urusi kuwekeza katika mpango wa miundomsingi wa Sh5.2 trilioni katika kipindi cha miaka 10, akilenga kuimarisha biashara kati ya mataifa hayo.

Akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara wa Kenya na Urusi mjini Moscow, Dkt Ruto alisema uwekezaji huo utasaidia kukuza viwanda, kuunda nafasi za kazi na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Alitaja sekta za nishati, uzalishaji wa mbolea, kilimo, usafiri, uchimbaji na uchakataji wa madini pamoja na utengenezaji wa bidhaa kuwa maeneo yanayohitaji uwekezaji.

Rais alisema Kenya inataka kuacha kuuza malighafi na kununua bidhaa zilizokamilika, akihimiza wawekezaji kuanzisha viwanda nchini na kutumia Kenya kufikia masoko ya Afrika.

Biashara kati ya mataifa hayo ilifikia takriban Sh49.38 bilioni mwaka 2025. Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh6.76 bilioni, hasa chai, kahawa, maua, matunda na mboga.

Dkt Ruto pia alitaja fursa katika kawi ya jotoardhi na magari yanayotumia umeme. Alisema asilimia 93 ya umeme nchini unatokana na vyanzo vinavyoweza kufanywa upya.

Alisisitiza kuwa soko la Afrika, la watu bilioni 1.5 kupitia Mkataba wa Biashara Huria wa Bara la Afrika, linaweza kuwapa wawekezaji fursa kubwa ya kupanua biashara zao.

Alisema Kenya inataka ushirikiano unaojenga viwanda, kuhamisha teknolojia na kuleta manufaa kwa pande zote.