HabariHabari za Kitaifa

Wakenya wapatao 4,000 waliangamia barabarani kati ya Januari na Oktoba – NTSA

Na HILARY KIMUYU October 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

KENYA imepoteza takriban watu 4,000 katika ajali za barabarani ndani ya miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, huku Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) ikitaka hali hiyo itangazwe janga la kitaifa.

Takwimu za NTSA zinaonyesha kuwa watu 3,995 walifariki kati ya Januari 1 na Oktoba 4, 2026, ongezeko la asilimia 9.2 ikilinganishwa na vifo 3,657 vilivyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Watembea kwa miguu ndio walioathirika zaidi, wakifuatwa na waendesha pikipiki. Kati ya waliofariki, watembea kwa miguu walikuwa 1,490, waendesha pikipiki 1,061, abiria 662 na madereva 352.

Mamlaka hiyo pia imetambua maeneo zaidi ya 270 hatari kwa ajali nchini, yakiwemo 199 katika Barabara Kuu ya Mombasa-Malaba.

Wito huo unafuatia ajali mbaya ya Oktoba 25 eneo la Kanga, karibu na Mtito Andei, ambapo watu 24 walifariki baada ya basi kugongana na lori. Ajali nyingine katika eneo la Salama mnamo Oktoba 3 ilisababisha vifo vya watu 17, wengi wao wakiwa waumini Wakatoliki.

Mkurugenzi wa Usalama Barabarani wa NTSA, Andrew Kipalgat, alisema kukabiliana na ajali kunahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa serikali na mashirika husika.

Alitaja hali ya magari na barabara, tabia za watumiaji na huduma za dharura kuwa mambo yanayopaswa kuchunguzwa.

Ripoti ya Utafiti wa Kiuchumi ya KNBS ya 2026 inaonyesha kuwa watu 5,009 walifariki katika ajali zilizoripotiwa mwaka 2025, ikilinganishwa na 4,748 mwaka 2024.

Sababu zinazochangia ajali ni pamoja na mwendo wa kasi, kupita magari kiholela, uchovu wa madereva, ulevi, magari yasiyofaa barabarani na miundombinu duni.

NTSA inasema kutangaza usalama barabarani kuwa janga la kitaifa kunaweza kusaidia kuratibu rasilimali na kuimarisha hatua za kupunguza vifo. Hata hivyo, mafanikio yatategemea ufadhili wa kutosha, utekelezaji wa sheria na ukarabati wa maeneo hatari.