Bunge lakataa sajili ya wapigakura ikaguliwe kabla ya uchaguzi wa 2027
JUHUDI za kuhakikisha sajili ya wapigakura inakaguliwa kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 zimepata pigo baada ya Bunge la Kitaifa kuondoa sharti la kisheria lililohitaji zoezi hilo lifanyike.
Mnamo Oktoba 22, 2026, wabunge walikataa pendekezo la Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi la kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuajiri kampuni huru na yenye sifa kufanya ukaguzi wa sajili hiyo miezi sita kabla ya uchaguzi.
Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma aliongoza upinzani dhidi ya pendekezo hilo, akisema lingepandisha gharama bila sababu.
Alisema majukumu yaliyopendekezwa tayari yanatekelezwa na IEBC chini ya Kifungu cha 8 cha Sheria ya Uchaguzi.
“Kwa nini IEBC iwe na jukumu la kusimamia sajili, kuikagua na kuirekebisha, kisha tutumie pesa za walipa ushuru kulipa kampuni nyingine?” aliuliza Bw Kaluma.
Hata hivyo, Bw Omondi alisema ukaguzi huru ni muhimu kwa uwazi na uwajibikaji, hasa katika kuthibitisha idadi ya wapigakura waliofariki na kuhakikisha majina yao yanaondolewa kwenye sajili.
Alisema IEBC husajili wapigakura, huku usajili wa vifo ukifanywa na taasisi nyingine huru. Kwa hivyo, kampuni isiyohusishwa na taasisi hizo mbili inapaswa kulinganisha rekodi na kuwaeleza Wakenya ni nani anayestahili kubaki kwenye sajili.
“Katiba yetu inahitaji uwazi na inaweka mifumo mbalimbali ya uwajibikaji,” alisema Bw Omondi.
Pendekezo lake lilitaka kampuni itakayoteuliwa kuwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa IEBC ndani ya siku 30. Tume hiyo pia ingetakiwa kuchapisha ripoti hiyo kwenye tovuti yake na kuiwasilisha kwa Bunge la Kitaifa na Seneti ndani ya siku 14 baada ya kuipokea.
Kukataa ukaguzi huo kunazua wasiwasi kutokana na matokeo ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya KPMG kabla ya uchaguzi wa 2022.
Ripoti hiyo ilitambua wapigakura 246,465 waliofariki lakini majina yao bado yalikuwa kwenye sajili. Pia ilipata rekodi 481,711 zilizokuwa na nambari za vitambulisho au pasipoti zilizorudiwa au kukosekana kwa taarifa muhimu.
Zaidi ya watu 226,000 walikuwa wamesajiliwa kwa kutumia vyeti ambavyo havikulingana na majina yaliyokuwa kwenye sajili. Ukaguzi huo pia ulifichua kuwa wafanyakazi 25 wa zamani wa IEBC walifikia sava za tume hiyo japo hawakuwa wameidhinishwa.
Wasiwasi kuhusu wapigakura waliofariki uliongezeka baada ya IEBC kumhoji Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar Hassan kufuatia matamshi yake katika mkutano wa kisiasa Mombasa mnamo Septemba 11, 2026.
Bw Omar alisema hata mtu akifa, kidole chake kinaweza kuchukuliwa na kutumika kwenye mfumo wa BVR kupiga kura. Baadaye alieleza tume hiyo kuwa matamshi hayo yalikuwa lugha ya kisiasa iliyolenga kuhamasisha wapigakura, wala hayakuwa na nia ya udanganyifu.
Mbunge Aden Mohammed wa Wajir Mashariki, aliyekuwa akiongoza Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa 2024, pia alipinga pendekezo la Bw Omondi akisema lingeongeza majukumu ya IEBC.
Bw Kaluma alitaja mapendekezo ya Tume ya Kriegler, iliyoshauri kuepukwa kwa marekebisho makubwa ya sheria za uchaguzi mwaka mmoja kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, mswada huo ulifikishwa Bunge la Kitaifa Februari 2025, baada ya kupitishwa na Seneti Desemba 2024.
Mswada huo sasa unarejea Seneti kwa kuangaliwa upya, hatua inayotoa nafasi ya sharti la ukaguzi kurejeshwa kupitia maafikiano kati ya mabunge hayo mawili.