Habari za KitaifaKimataifa

Mataifa yaheshimu mipaka na mamlaka ya kila nchi – Ruto

Na MERCY SIMIYU October 30th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ametoa wito kwa mataifa yote kuheshimu mamlaka na mipaka ya nchi nyingine bila kujali ukubwa au nguvu zake, akisisitiza kuwa mizozo ya kimataifa inapaswa kutatuliwa kwa njia za amani.

Akizungumza Alhamisi, Oktoba 29, katika Mkutano wa Tatu wa Urusi na Afrika mjini Moscow, Urusi, Dkt Ruto alisema uhusiano wa kimataifa unapaswa kujengwa kwa kuheshimiana badala ya mataifa yenye nguvu kutaka kutawala maeneo ya nchi nyingine.

Alisema kanuni za usawa wa mataifa, kuheshimu mipaka na kutatua mizozo kwa amani zinapaswa kutumika kwa kila nchi bila ubaguzi.

Rais pia alitaka mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema Afrika yenye watu 1.6 bilioni na mataifa 54 haiwezi kuendelea kukosa uwakilishi wa kudumu katika chombo hicho muhimu.

Alisema mfumo wa utawala wa dunia unapaswa kuakisi hali ya sasa badala ya kuendelea kutegemea mipango iliyowekwa mwaka 1945 baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Kenya inaunga mkono msimamo wa pamoja wa Afrika unaotaka bara hilo kupewa viti vya kudumu katika baraza hilo, pamoja na haki inayofurahiwa na wanachama wa sasa.

Katika masuala ya uchumi, Dkt Ruto alisema Afrika inapaswa kuacha kutegemea kuuza malighafi na kununua bidhaa zilizokamilika,  na badala yake iwekeze katika viwanda, teknolojia na kuongeza thamani ya bidhaa.

Alialika kampuni za Urusi kuwekeza katika viwanda vya Afrika, kuhamisha teknolojia na kutoa mafunzo ya kiufundi yatakayosaidia vijana kupata ajira.

Alitaja kilimo, uzalishaji wa mbolea, unyunyuzaji, usindikaji wa mazao, nishati, afya na utengenezaji wa dawa kuwa maeneo muhimu ya ushirikiano.

Rais Ruto pia alitaka mataifa tajiri kutoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa masharti nafuu, akisema Afrika inaathiriwa na ukame, mafuriko na uhaba wa chakula licha ya kuchangia kidogo katika uzalishaji wa gesi chafu.

Aidha, alitaka mageuzi katika mifumo ya ufadhili wa kimataifa ili nchi zinazoendelea zipate mikopo nafuu na fedha kwa miundomsingi na viwanda.

Alisema mpango wa ushirikiano wa Urusi na Afrika wa 2027–2029 unapaswa kuzaa matokeo yanayopimika, yakiwemo uwekezaji, ajira, tafiti na viwanda vitakavyoboresha maisha ya wananchi.