Wakimbizi kutoka Ethiopia waliopenya Kenya wazidi 50,000 vita vikichacha
IDADI ya raia wa Ethiopia wanaokimbilia Kenya kupitia Moyale kutokana na mapigano katika nchi hiyo jirani imezidi 50,000, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Idadi hiyo imeongezeka kutoka takriban 40,000 mwishoni mwa wiki huku mapigano kati ya vikosi na wanamgambo wa maeneo ya Oromia na Somali nchini Ethiopia yakiingia siku ya nane.
UNHCR ilisema wanawake na watoto ndio wengi miongoni mwa waliotoroka makazi yao. Baadhi wamepata hifadhi kwa jamaa na wenyeji, huku wengine wakilala katika shule na makanisa.
Shirika hilo lilitaja chakula kuwa hitaji la dharura, likiongeza kuwa wakimbizi wanahitaji maji safi, makazi ya muda, huduma za afya na usafi.
Naibu Kamishna wa Kaunti ya Moyale, Benedict Munywoki, alisema idadi ya wanaovuka mpaka inaendelea kuongezeka kutokana na milio ya risasi inayosikika mara kwa mara.
Alisema tathmini ilikuwa ikiendelea kubaini idadi kamili ya walioingia nchini, huku mashirika ya kutoa misaada yakishirikiana kuwahudumia.
UNHCR inashirikiana na Idara ya Huduma za Wakimbizi nchini, serikali ya Kaunti ya Marsabit, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya na mashirika mengine kuandaa misaada ya dharura kwa karibu watu 12,000.
Shirika hilo pia linasema juhudi zinaendelea kuhamisha kambi za wakimbizi kutoka maeneo yaliyo karibu na mpaka ili kuimarisha usalama wao.
Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, alisema polisi na wanajeshi wa Kenya wameongeza doria mjini Moyale na maeneo ya mpakani kuhakikisha usalama.
Wakati huohuo, watu saba wanachunguzwa kwa madai ya kusambaza matamshi ya chuki na kuchochea mizozo ya jamii kupitia mitandao ya kijamii.
Bw Kamande aliwataka Wakenya kujiepusha na kauli zinazoweza kuongeza mvutano.