Vigogo wageuza mikakati kuelekea 2027, watua vijijini naTikTok kujipigia debe
CHINI ya mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, wanasiasa wanaowania urais na vyama vyao vya kisiasa wamebadili mbinu zao, wakielekeza nguvu katika vijiji na maeneo ya mashambani kuwafikia wapiga kura.
Badala ya kutegemea mikutano mikubwa katika miji na ushawishi wa vigogo wa kisiasa, viongozi wameanza kuingia katika vijiji vidogo, vibanda vya biashara na makazi ya kawaida ili kujenga uhusiano wa karibu na wananchi.
Rais William Ruto na viongozi wa upinzani wameongeza ziara za mashinani, wakijitahidi kuwashawishi wapiga kura moja kwa moja kabla ya kampeni rasmi kuanza.
Rais Ruto, anayelenga muhula wa pili, ameonekana akila katika vibanda vya kando ya barabara, kuingia manyattani na kutembelea nyumba za kawaida za mashambani.
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, ametembelea zaidi ya kaunti 20 na kuandaa mikutano ya hadhara zaidi ya 50 katika maeneo mbalimbali.
Katika ziara zake za Narok na Kajiado Agosti na Septemba 2026, alitembelea maeneo ya mashambani yakiwemo Olokurto, Olpusimoru, Ololulung’a na Ewaso Ng’iro, kabla ya kuelekea Rombo, Loitokitok, Namanga na Kimana.
Pia ametembelea maeneo ya mbali ya Pokot Magharibi, yakiwemo Sigor, Kacheliba na Kapenguria, akizindua miradi na kuwahimiza wafuasi wake kujiandikisha kupiga kura kwa wingi.
Katika Ukambani, alitembelea Mwingi, Kitui West, Kibwezi, Matuu na Mwala. Mwingi Kaskazini, nyumbani kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, alikagua mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Tseikuru, akazindua barabara na kutoa hati za kumiliki ardhi.
Ziara hizo pia zimefika Pwani, Magharibi na Nyanza, maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa ngome za upinzani.
Rais ametembelea kaunti za Kisumu, Migori, Siaya na Homa Bay, akitangaza miradi ya masoko, maji, umeme na elimu.
Katika ziara ya Pwani iliyochukua siku nane, alitembelea Taita Taveta, Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River, ambako alisimamia utoaji wa karibu hati 200,000 za kumiliki ardhi.
Upinzani nao haujachelewa. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ametembelea kaunti 15 katika miezi mitatu, akiandaa mikutano 36 ya mashinani.
Vuguvugu la Linda Mwananchi, linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pamoja na Mbunge Babu Owino na Seneta Godfrey Osotsi, limefanya mikutano sita katika Nyanza, Magharibi na Pwani.
Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha Rigathi Gachagua kimefanya mikutano 24 katika kaunti mbalimbali, zikiwemo Nakuru, Nyandarua, Laikipia, Kiambu, Kajiado, Nyeri na Murang’a.
Mchambuzi wa siasa Profesa XN Iraki anasema mbinu hiyo inaweza kumsaidia Rais Ruto kwa sababu kukutana ana kwa ana na wapiga kura huwafanya wamzoee na kujenga uhusiano naye.
Hata hivyo, Dkt Peter Mbae wa DCP anasema ziara hizo huenda zisibadilishe hisia za wananchi wanaokabiliwa na gharama kubwa ya maisha, mzigo wa ushuru na ahadi za kampeni ambazo hazijatekelezwa.
Mchambuzi mwingine, Profesa Tom Nyamache, anasema Pwani, Magharibi, jamii ya Maa na Turkana zitasalia kuwa maeneo muhimu katika uchaguzi huo.
Wakati huohuo, wataalamu wa utawala wanaonya kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana unaweza kuwafanya washawishike kutumiwa vibaya kisiasa au kuhusishwa na ghasia za uchaguzi.
Mbali na mikutano ya mashinani, mitandao ya kijamii kama TikTok, Facebook, X na WhatsApp inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kampeni za 2027.
Mwanasheria na mchambuzi wa sera Steve Kabita anasema mitandao hiyo itakuwa jukwaa kuu la kujenga mitazamo ya kisiasa na kushawishi wapiga kura.
Mwanaharakati Morara Kebaso anasema wapiga kura wa 2027 watakuwa na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya kisiasa kutokana na elimu ya uraia na matumizi ya teknolojia.
Ripoti ya Thomson Reuters Foundation pia inaonyesha kuwa mitandao ya kijamii itakuwa na nafasi kubwa katika uchaguzi ujao, huku kampeni zikielekea zaidi kwenye majukwaa ya kidijitali.
Hata hivyo, viongozi wa kijamii na kidini wanawahimiza wananchi kutathmini sera, mipango ya maendeleo na uwezo wa wagombeaji kutatua matatizo yao badala ya kushawishiwa na umaarufu au misimamo ya vyama.