Njama ya ODM kufyeka waasi ikijipanga kwa kura za 2027
CHAMA cha ODM kimeanza mkakati wa kupunguza ushawishi wa viongozi wanaokiasi au kukosa uaminifu kwake, huku kikisisitiza kuwa uteuzi wa wagombeaji kuelekea uchaguzi wa 2027 utakuwa huru na wa haki.
Mabadiliko ya kisiasa yanayoshuhudiwa ndani ya chama hicho yanawaweka viongozi kadhaa katika hatari ya kupoteza tiketi za ODM baada ya wapinzani wao kujiunga na chama hicho.
Kiongozi wa chama, Dkt Oburu Oginga, amekuwa akitaka wanachama kuonyesha uaminifu usio na masharti.
Uamuzi wa Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja kujiunga na ODM umevuruga mipango ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, ambaye alihama na kujiunga na chama cha Mwananchi akinuia kutumia tiketi yake kuwania ugavana.
Sakaja amesisitiza kuwa hakujiunga na ODM ili kuchukua nafasi ya mtu mwingine, bali kutwaa nafasi anayostahili.
Hata hivyo, Owino alikuwa amedai uongozi wa chama ungependekeza Sakaja kuwania ugavana na hivyo kukosa uteuzi wa haki.
Eneo la Suba Kaskazini, Mbunge Millie Odhiambo anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Silas Jakakimba, aliyekuwa msaidizi wa marehemu Raila Odinga, ambaye amerejea ODM kutoka UDA.
Jakakimba amekuwa akihamasisha wafuasi kwa kauli mbiu ya Diet nyaka loki, akimaanisha kuwa lazima uongozi ubadilike.
Anatarajiwa kupambana na Odhiambo katika mchujo wa chama.
Katika Suba Kusini, Mbunge Caroli Omondi ameihama ODM, huku mpinzani wake wa uchaguzi wa 2022, Stephen Sangira, akijiunga na chama hicho.
Sangira anasema yuko tayari kuwania kiti hicho kwa tiketi ya ODM.
Eneo la Kitutu Chache Kusini, ODM imempokea msomi Dkt Andrew Maubi kama mpinzani kumkabili Mbunge Anthony Kibagendi, ambaye amejiunga na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i.
Jijini Nairobi, chama hicho pia kimempokea aliyekuwa Mbunge wa Embakasi Magharibi, George Theuri, anayelenga kumng’oa mbunge wa sasa Mark Mwenje.
Mwenje amehamia DCP ya Rigathi Gachagua.
Mabadiliko hayo yanaonyesha kuwa ODM inajaribu kurejesha nguvu katika maeneo ambayo hapo awali ilikubali kutokuwa na wagombeaji chini ya makubaliano ya kisiasa.
Hata hivyo, vita vya tiketi za chama vinaweza kuongeza ushindani na migawanyiko ndani ya ODM, huku viongozi wapya na wa zamani wakipigania nafasi ya kuwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa 2027.