Mackenzie kuishi jela miaka 200 kutokana na vifo Shakahola
KIONGOZI wa dhehebu la Good News International (GNI), Paul Nthenge Mackenzie, amehukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 200 gerezani kwa mauaji ya watoto 190 na mtu mzima mmoja katika msitu wa Shakahola kati ya Januari 2021 na Septemba 2023.
Jaji Diana Kavedza akiwa katika Mahakama Kuu mjini Mombasa, alimpa Mackenzie vifungo viwili tofauti vya miaka 100 kila kimoja, kutegemea jinsi waathiriwa walivyofariki.
Kifungo cha kwanza kinahusu vifo vya watu 183, wakiwemo watoto 182 na mtu mzima mmoja, waliokufa kwa njaa baada ya kunyimwa chakula. Mackenzie alihukumiwa miaka 100 kwa kila shtaka kati ya mashtaka hayo 183, lakini vifungo hivyo vitaendelea kutekelezwa kwa wakati mmoja.
Kifungo cha pili kinahusu watoto wanane waliouawa moja kwa moja kwa kunyongwa, kubanwa shingo, kukosa hewa au kupigwa kwa vitu butu. Mackenzie alipewa miaka 100 kwa kila shtaka kati ya hayo manane, huku vifungo hivyo pia vikitumika kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, jaji aliamuru vifungo hivyo viwili vikuu vitekelezwe kwa kufuatana, hivyo kufikisha jumla ya miaka atakayokuwa gerezani kuwa 200.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Kavedza alisema mauaji ya Shakahola yalipangwa mapema na kuendelea kwa muda mrefu, hivyo adhabu ilipaswa kuonyesha uzito wa uhalifu huo.
“Adhabu ya mahakama hii lazima ilingane na giza la matendo yao na kiwango cha juu cha adhabu kinachoruhusiwa na sheria,” alisema.
Jaji huyo alieleza namna watoto wadogo walivyoteseka mikononi mwa watu waliopaswa kuwalinda. Wengi wao walikuwa wakitegemea wazazi na walezi wao, lakini walinyimwa chakula, maji na ulinzi kwa makusudi.
Alisema baadhi ya waliopatikana na hatia hawakuonyesha majuto, huku wakiendelea kusisitiza kuwa watoto wao wako mbinguni na wao pia wako tayari kuwafuata.
“Wahalifu wamesimama bila hata kuinamisha shingo, hawana hatia moyoni wala majuto, wakitangaza kwa imani yao potovu na kiburi kuwa watoto wao wako mbinguni na wako tayari kuwafuata. Je, watu wa aina hii wanastahili hata chembe ya huruma? Je, haki inapaswa kulegeza msimamo na kuonyesha huruma mahali ambapo huruma ilifutwa kwa utaratibu? Hapana,” alisema.
Jaji Kavedza alisema watoto walilemazwa na kunyimwa haki zao kwa kisingizio cha dini, huku baadhi ya manusura wakiachwa yatima na kuishi katika vituo vya watoto, ambako walezi wamekuwa wazazi wao wapya.
Alisema adhabu nafuu isingeweza kurekebisha madhara ya kudumu yaliyosababishwa na mauaji hayo.
Mahakama ilimtambua Mackenzie kama mpangaji mkuu wa mauaji hayo kutokana na nafasi yake kama kiongozi wa GNI na makazi ya wafuasi wake katika msitu wa Shakahola.
Katika tathmini ya jukumu lake, jaji alisema Mackenzie ndiye aliyewaongoza wafuasi wake kuhamia msituni na kuendesha mikutano ambako aliwaagiza wafunge hadi wafe. Pia aliagiza watoto wawe wa kwanza kufa kwa njaa.
Mahakama ilisema Mackenzie alisimamia mazishi aliyoyaita harusi, akitoa maagizo kwa wazee wa vijiji kupitia naibu wake Smart Deri Mwakalama. Pia aliamuru matumizi ya nguvu dhidi ya watoto waliokataa kufunga, waliotaka kuacha zoezi hilo au kujaribu kutoroka.
Jaji alisema adhabu haikupaswa kuzingatia tu idadi ya waliouawa, bali pia mateso waliyopitia kabla ya kufariki.
“Sheria haitoi adhabu kwa nia ya kulipiza kisasi, bali kwa sababu ya kuzuia uhalifu usijirudie. Ni onyo kali kwa binadamu wote kuwa hakuna shupavu wa imani wala kiongozi katili aliye na haki ya kuua, na yeyote atakayejaribu atahisi uzito wa mkono wa mahakama,” alisema.
Mahakama ilipanga waathiriwa kulingana na umri na sababu zilizothibitishwa za vifo vyao, huku ikizingatia udhaifu wao na mazingira waliyokufa.
Kati ya waathiriwa 191, watoto 161 walikuwa watoto wachanga wanaoanza kutembea na walio chini ya umri wa miaka tisa na nusu. Wengine 22 walikuwa na umri wa miaka 10 hadi 13, watano walikuwa na miaka 14 hadi 16 na nusu, huku umri wa watoto wawili ukishindwa kubainika. Mtu mmoja alikuwa mtu mzima.
Kisa cha mtoto mchanga aliyekuwa na siku 12 pekee kilimgusa jaji, ambaye alieleza mateso aliyopitia kabla ya kufariki.
“Fikiria mtoto mchanga, maisha madogo yaliyokuwa na siku 12 tu duniani, aliyenyimwa maziwa ya mama tangu kuzaliwa, kitovu chake kikiwa bado hakijapona, akaachwa akinyauka kwenye joto kali huku wale waliokuwa wakisimamia zoezi hilo wakitazama. Siku 12 za kilio dhaifu kilichopungua hadi pumzi ya mwisho,” alisema.
Watoto wengine 161 walikufa taratibu kutokana na njaa na kiu. Mahakama ilisema walilia wakitafuta chakula na maji, lakini badala ya kusaidiwa walikutana na ukatili kutoka kwa watu waliopaswa kuwalinda.
Jaji alitaja maagizo yaliyohusishwa na Mackenzie kwamba watoto wangeingia mbinguni kupitia “mangumi na mateke.”
Watoto 22 wenye umri wa miaka 10 hadi 13 walikuwa na uwezo wa kuelewa usaliti wa wazazi wao, lakini hawakuwa na nguvu za kutoroka mateso hayo.
Vijana watano waliokuwa na umri wa miaka 14 hadi 16 na nusu walipinga maagizo ya kufunga hadi kufa. Mahakama ilisema baadhi yao walifungwa mikono, kufungiwa ndani, kupigwa kwa vitu butu na kunyongwa.
Jaji alisema wale waliojaribu kupigania maisha yao walikabiliwa kwa ukatili badala ya kulindwa.
Katika kutoa adhabu, mahakama ilizingatia haja ya kuzuia uhalifu kama huo, kutoa haki kwa waathiriwa na kulinda jamii dhidi ya watu wanaowadhuru walio dhaifu.
Hata hivyo, jaji alisisitiza kuwa kila mshtakiwa alipaswa kuhukumiwa kulingana na nafasi yake, kiwango cha ushiriki na jukumu lake katika mauaji hayo.
Naibu wa Mackenzie, Smart Deri Mwakalama, alihukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 160.
Washtakiwa wengine walipata vifungo vya kati ya miaka 100 na 160 kwa makosa yanayohusiana na mauaji hayo.