Habari

Mapuuza ya serikali kuhusu Mackenzie yaliyochangia mauaji Shakahola

Na Steve Otieno November 7th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KWA miaka saba, shughuli za mhubiri Paul Mackenzie zilizohusishwa na itikadi kali na vifo vya wafuasi wake zilikuwa zikijulikana na polisi, maafisa wa mahakama, kamati za usalama na mashirika ya kulinda watoto. Hata hivyo, hatua madhubuti hazikuchukuliwa hadi makaburi ya halaiki yalipogunduliwa katika msitu wa Shakahola.
Ripoti za watu kupotea, watoto kunyimwa elimu na familia kutengana zilikuwa zimewasilishwa kwa mamlaka mbalimbali. Lakini wafuasi wa Mackenzie waliendelea kuingia msituni, ambako mamia yao walikumbana na njaa, mateso na kifo.
Kamati maalumu ya Seneti iliyochunguza mkasa huo ilisema katika ripoti yake ya Oktoba 19, 2023 kuwa kulikuwa na fursa nyingi za kuokoa maisha, lakini idara za serikali zilishindwa kuunganisha taarifa na kuchukua hatua.
Mackenzie alikuwa akiwaagiza wafuasi wake kuacha kazi, kukataa matibabu na kupinga baadhi ya mipango ya serikali kama vile sensa, kampeni za kutoa dawa za minyoo na Huduma Namba.
Kamati ya usalama ya Kaunti ya Kilifi iliwahi kumwita kueleza mafundisho yake na madai ya kuwatesa wafuasi. Maafisa walimuonya kuhusu mafundisho hayo, lakini hawakuchukua hatua zaidi.
“Ushahidi uliowasilishwa kwa Kamati unaonyesha kuwa Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Kilifi ilikuwa na taarifa za awali kuhusu shughuli za Paul Mackenzie lakini ilikosa kuchukua hatua,” ripoti hiyo ilisema.
Mwaka 2022, Mackenzie alidai kuwa alikuwa mkulima na alikuwa ameacha kazi ya kuhubiri. Seneti ilikosoa serikali kwa kutofuatilia madai hayo.
Mackenzie alikuwa amewahi kukabiliwa na mashtaka mbalimbali. Mnamo Machi 14, 2017, alishtakiwa kwa kuendesha shule isiyosajiliwa katika kanisa lake la Good News International Ministries mjini Malindi. Alikubali makubaliano na upande wa mashtaka, akatozwa faini ya Sh20,000 na kuagizwa kuwa na tabia njema.
Mnamo Oktoba mwaka huo huo, alishtakiwa tena kwa kueneza itikadi kali, kuendesha shule bila usajili, pamoja na kuwanyima watoto elimu. Hata hivyo, aliachiliwa huru Oktoba 29, 2021 kutokana na ukosefu wa ushahidi.
Mwaka huo, watoto 43 wenye umri wa mwaka mmoja hadi 13, wakiwemo watatu wa Mackenzie, waliokolewa kutoka kanisa lake Mayungu. Walikuwa wakinyimwa elimu na kupewa mafundisho yake yenye itikadi kali.
Mwaka 2019, Kamati ya Watumiaji wa Mahakama ya Kaunti ya Kilifi ilijadili madai ya watoto kuingizwa katika itikadi kali kupitia kanisa na kituo cha televisheni cha Mackenzie. Suala hilo lilipelekwa kwa kamati ya kitaifa na Mamlaka ya Mawasiliano. Leseni ya kituo hicho ilifutwa, lakini kamati haikufahamishwa kuhusu pendekezo la kulifuta kanisa.
Ishara nyingine muhimu ilitolewa Machi 6, 2022, wakati taarifa ya kupotea kwa Sylvia Adoyo Mwende ilipotolewa katika Kituo cha Polisi cha Likoni. Inadaiwa alikuwa amepelekwa Shakahola baada ya kumtembelea Mackenzie.
Konstebo Wilson Lekaken aliyekuwa akichunguza kisa hicho alisema alipata kibali cha mazishi kwa jina la Sylvia pamoja na maandishi yaliyodokeza alikuwa amefariki Shakahola na kuzikwa bila mwili kupelekwa mochari.
Hata hivyo, maswali yaliibuka kuhusu iwapo kibali hicho kilithibitishwa na chifu msaidizi aliyedaiwa kukitoa na kama kaburi lilichunguzwa au mwili kufukuliwa.
Mnamo Machi 2023, Francis Wanje aliyekuwa akitafuta wajukuu wake alipata amri ya mahakama ya kufukua miili ya watoto wawili waliodhaniwa kuzikwa msituni. Polisi walichukua siku tano kufika eneo hilo baada ya taarifa kutolewa kuhusu mvulana wa miaka minane na makaburi yaliyoshukiwa kuwemo
Maafisa walioandamana na Wanje na Victor Kaudo wa Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Malindi wanadaiwa kupokea simu na kuondoka, wakiwaacha raia hao wawili. Seneti haikuweza kubaini aliyepiga simu hiyo.
Amri ya kufukua miili iliyotolewa Machi 21, 2023 ilitekelezwa Aprili 14, wakati ukubwa wa mkasa huo ulipoanza kufahamika