Karata ya Gachagua kwa Kalonzo, Sifuna kuelekea 2027
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anajaribu kujenga muungano mpana wa upinzani utakaompa nafasi muhimu katika uchaguzi wa urais wa 2027. Hata hivyo, mpango wake wa kuunganisha maeneo yenye kura nyingi unakabiliwa na mvutano kuhusu nani atakayeongoza, nani atakayetoa kura na ni nani atakayekuwa na usemi mkubwa katika kugawana mamlaka.
Kutoka nyumbani kwake Wamunyoro, kiongozi huyo wa Democracy for the Citizens Party (DCP) anauza ujumbe wa mashauriano, ushirikiano na umoja wa upinzani. Lakini nyuma ya ujumbe huo kuna mkakati mkali unaoitwa Operation Okoa Kenya, unaolenga kuunganisha maeneo yenye ushawishi wa kisiasa, kupunguza ushawishi wa Rais William Ruto na kuwalazimisha wapinzani kujadiliana wakiwa na nguvu za kutosha.
Kiini cha mpango huo ni muungano unaopendekezwa kati ya DCP ya Gachagua, Wiper ya Kalonzo Musyoka na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Edwin Sifuna. Mlima Kenya, Ukambani, Magharibi na Nyanza ndizo nguzo kuu za kisiasa zinazotarajiwa kuunda muungano huo.Gachagua aliambia Taifa Jumapili kuwa mpango utaanza kwa kuunganisha maeneo ya kijiografia, huku DCP na Wiper zikimsaidia Sifuna kupata uungwaji mkono katika maeneo yaliyokuwa ngome za marehemu Raila Odinga.
“Unaanza na maeneo. Makubaliano ni kwamba DCP na Wiper zitasaidia vuguvugu la Linda Mwananchi la Edwin Sifuna kupata uungwaji mkono katika ngome za jadi za Raila Odinga, hasa Magharibi na Nyanza,” alisema.Alisema baada ya Sifuna kuimarisha maeneo hayo, wataungana na Mlima Kenya na Mashariki, kisha kuimarisha Nairobi na Pwani ili kuunda muungano wenye uwezo wa kushindana na Kenya Kwanza.
Kaimu Katibu Mkuu wa DCP John Methu anasema mkakati huo unalenga kujenga ukuta wa kisiasa utakaowazuia washirika wa Rais Ruto kufanya kampeni kwa urahisi katika maeneo hayo.Anasema mpango huo hautahusu tu mazungumzo ya kugawana nafasi za uongozi, bali pia kutambua na kuidhinisha mapema wagombea wenye nguvu ili kukabiliana na washirika wa serikali.
“Ukuta huo utajengwa mashinani. Mpango ni kuwatangaza na kuwaidhinisha mapema wagombea wenye nguvu, hata kama hawatashinda mara moja, ili kujenga upinzani endelevu dhidi ya washirika wa Ruto,” alisema Methu.
Katika Magharibi, Gachagua anataka washirika wa Rais Ruto, akiwemo Farouk Kibet, Francis Atwoli, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula, wakabiliwe na upinzani uliopangwa.Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, ambaye anaongoza kampeni za urais za Sifuna, anasema lengo ni kumzuia Ruto kurithi kura za Raila.“Gachagua ana silaha kuu ambayo ni kura za Mlima Kenya zilizomfanya Dkt Ruto kuwa rais mwaka 2022.

Sifuna na Musyoka ndio watakaomzuia Ruto kurithi kura za Raila. Tunataka kumzuia Ruto asipate zaidi ya asilimia 30 ya kura alizopata mwaka 2022,” alisema.Hata hivyo, mkakati huo unamuweka Gachagua katika hali ngumu. Anahitaji kuonyesha kuwa anaweza kuunganisha Mlima Kenya, lakini eneo hilo limeanza kuwa uwanja wa mapambano kati ya wanasiasa wenye malengo tofauti.Mustakabali wake pia haujawa wazi baada ya Mahakama Kuu kukataa kubatilisha uamuzi wa Seneti uliomuondoa mamlakani.
Ingawa anaweza kukata rufaa, changamoto hiyo inatatiza juhudi zake za kujitangaza kuwa kiongozi asiye na mpinzani katika eneo hilo.Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema changamoto ya Gachagua si tu kuamua iwapo atawania urais, bali pia kujua atakayeunga mkono, jinsi ya kujadiliana kwa niaba ya Mlima Kenya katika serikali ijayo na jinsi ya kuzuia wapinzani wake eneo hilo kutwaa ushawishi aliojenga.
Gachagua pia anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Muturi na aliyekuwa Waziri Peter Munya, ambao wamekataa shinikizo kwamba vyama vidogo vya Mlima Kenya kuvunjwa na kujiunga na DCP. Wanasema ushirikiano haupaswi kumaanisha kupoteza utambulisho wa vyama vyao. Munya amehoji kwa nini mazungumzo ya muungano yanafanyika nyumbani kwa Gachagua Wamunyoro badala ya jukwaa lisiloegemea upande wowote.
Katika juhudi za kupanua ushawishi wake, Gachagua amefikia aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu, hatua inayotafsiriwa kama jaribio la kupunguza nguvu za Kalonzo katika Ukambani iwapo kiongozi huyo wa Wiper hatakubaliana na masharti yake.Mmoja wa maafisa wanaofahamu mazungumzo hayo anasema mkakati ni kutumia nguvu za kura za Mlima Kenya na Magharibi kujenga muungano wa kitaifa, huku Ngilu akisaidia kuvutia sehemu ya Ukambani iwapo Kalonzo hatakuwa tayari kufanya maelewano.
Hatua hiyo imezua wasiwasi ndani ya Wiper. Seneta wa Kitui Enoch Wambua ameshutumu Ngilu kwa kudhoofisha azma ya Kalonzo ya kuwania urais.Mratibu wa wagombea wa DCP Mlima Kenya Joseph Waweru anasema Gachagua anataka mazungumzo ya mwisho ya muungano yafanyike baada ya kura za mchujo za vyama Machi 2027, ili kila chama kijue nguvu yake kupitia wagombea kitakaowapata.
Lakini Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, mshirika wa Sifuna, anataka mgombea wa urais wa upinzani atangazwe kabla ya Desemba mwaka huu. Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri naye amewaonya Sifuna na Kalonzo dhidi ya kuingia katika muungano ambao unaweza kutumiwa na Gachagua kutanguliza maslahi yake.