• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Mahakama haitakuokoa, ODM yamwambia Jumwa

Mahakama haitakuokoa, ODM yamwambia Jumwa

CHARLES LWANGA na WANDERI KAMAU

CHAMA cha ODM kimesema kuwa katu hakitabatilisha uamuzi wa kumtia mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, kikisema kuwa hata korti haitamuokoa.

Mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi jana alisema ODM ‘imefunga ukurasa’ wa Bi Jumwa na kuwakashifu wanaokosoa uamuzi wa chama hicho.

Kinara wa chama hicho Raila Odinga vilevile alishikilia kuwa huo haukuwa uamuzi wake binafsi bali mchakato rasmi wa ODM na hauhusiana kwa vyovyote na ‘handisheki’

Wakati huo huo, baadhi ya wabunge na madiwani wa chama cha ODM katika Kaunti ya Kilifi wanaomuunga mkono Bi Jumwa wamekashifu hatua ya kumfurusha mbunge huyo chamani kwa madai ya kutokuwa mwaminifu na kukosa nidhamu.

Bi Jumwa tayari amepokea amri kutoka kwa mahakama ya migogoro ya vyama vya kisiasa (PPDT) inayoahirisha hutua hiyo ya kufurushwa kwake kutoka kwa chama cha ODM.

Baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakiunga mkono hatua za kisiasa za Bi Jumwa ni Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Michael Kingi (Magarini), Gertrude Mbeyu (mwakilishi wa wanawake) na mbunge wa Kaloleni Paul Katana.

Wabunge hao wanne pamoja na Bi Jumwa wamekuwa wakiandamana na naibu wa Rais William Ruto katika mikutano ya hadhara na michango wakiahidi kufanya kazi naye kwa ajili ya maendeleo na hata kupigia debe azma yake ya urais mwaka wa 2022.

Lakini, Bw Katana jana aliambia Taifa Leo kuwa uamuzi wa kufurushwa kwa Bi Jumwa itaathiri msimamo wa demokrasia wa chama akifafanua kuwa hatua ya Bi Jumwa kumuunga mkono Bw Ruto inatokana na mapatano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

“Aisha Jumwa amechangia pakubwa katika chama cha ODM, ni nani hajui ya kuwa Bi Jumwa alifungwa seli katika kituo cha polisi cha Pangani kwa siku kadhaa kwa sababu ya msimamo wake wa chama?” alisema na kuongeza “unakumbuka nyimbo kama vile ‘salama salama Jubilee’ ambazo aliziimba wakati wa kampeni?”

Kuhusu suala la kuunga azma ya urais Bw Ruto katika uchaguzi wa mwaka wa 2022, Bw Katana aliwaambia viongozi wazingatie masuala ya maendeleo ili waimarishe maisha ya wakazi badala ya kupiga siasa za 2022.

“Hakuna mtu ameandikiwa barua na Mungu ya kuwa 2022 atakuwa hai, lakini wakati huo ukifika tutafanya uamuzi wa mgombeaji bora wa urais kulingana na rekodi yake ya maendeleo,” alisema.

Wiki iliyopita, mbunge wa Magarini Michael Kingi ambaye pia alipigia debe azma ya urais ya Bw Ruto alisema kwamba msimamo wake wa kumuunga mkono Bi Jumwa hautabadilika kwa sababu chama cha ODM kilivunja sheria kwa kuamua kumwadhibu mbunge huyo wa Malindi.

Haya yaliungwa mkono na diwani wa Shella Adamson Kadenge ambaye pamoja na mwenzake wa ganda Abdulrahman Omar na Malindi Mjini David Kadenge wamekuwa wakiambatana na Bi Jumwa katika ziara zake za maendeleo.

Bw Kadenge ambaye pia ni kinara wa wengi katika bunge la Kilifi alishangaa ni kwa nini chama chao cha ODM kinamuadhibu Bi Jumwa huku ikimsameha mbunge wa Msambweni Suleiman Dori na madiwani wengine walioasi chama.

“Haki inafaa ifanywe kwa wote,” alisema na kuongeza “lakini endapo chama kimfurushe na tuwe na uchaguzi mdogo, nitamuunga mkono ambaye atasimamishwa na chama cha ODM.”

Bw Kadenge alisema uhusiano wake na Bi Jumwa, ambaye pia ni mwanachama wa ODM ni kwa ajili ya maendeleo na akakataa kuhusishwa na madai kuwa yuko miongoni mwa wanasiasa wanaompigia debe Bw Ruto azima yake ya urais 2022.

Bw upande mwengine, wabunge na madiwani ambao wanapinga Bi Jumwa kwa kuasi chama walimwabia abebe msalaba wake ambao amejitakia mwenyewe.

Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Kilifi alienda mtandaoni kumuomboleza Bi Jumwa baada kufurushwa chamani akimwabia apambane na hali yake.

Bw Mwambire ambaye amekuwa akikashifu wabunge wanaompigia debe azima ya urais ya Bw Ruto mwaka wa 2022 alisema Bi Jumwa alisalitiwa na wanasiasa wa pwani ambao walikosa kutangaza msimamo wao wa kisiasa rasmi, mwishowe wakasamehewa na chama.

Kwa upande wake, Bw Ken Chonga, mbunge wa Kilifi Kaskazini alisema kuwa uamuzi wa chama ilikuwa ya haki na funzo kwa wabunge wengine waasi.

“Ikiwa anasema chama cha ODM hakina hakim bona anaenda mahakamani kupinga kufurushwa chamani? Si aende tu atafute chama kingine cha haki badala ya kugwamia ODM?” alisema.

Diwani wa Kakuyuni Nixon Muramba pamoja na mwenzake wa Jilore Daniel Chiriba halmaarufu Bonyeza ambao walikosana na Bi Jumwa kisiasa baada ya uchaguzi mkuu uliyopita walimwambia Bi Jumwa awachane na kupambana na chama mahakamani na badala yake aende kwa uchaguzi.

Bw Muramba ambaye ana nia ya kunyakuwa kiti hicho endapo kitabaki wazi baada ya Bi Jumwa kufurushwa alisema atatafuta ruhusa kwa chama cha ODM kabla ya kufanya uamuzi kamili.

“Nitatafuta maoni ya chama na wakazi wa Kakuyuni ambao ninawaakilisha kabla ya kuwania kiti cha Malindi endapo kitabaki huru,” alisema.

You can share this post!

Kiwanda cha Kibos hatarini kufungwa

Wanawake nyota waliong’aa katika fani mbalimbali

adminleo