• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
KANU yaanza kupenya Mlima Kenya kumzima Ruto

KANU yaanza kupenya Mlima Kenya kumzima Ruto

NA JOSEPH WANGUI

CHAMA cha KANU kimeanza rasmi mchakato wa usajili wa maajenti 10,000 katika kaunti 10 za ukanda wa Mlima Kenya kinapolenga kujizolea umaarufu katika ngome hiyo ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuzima umaarufu wa Naibu Rais Dkt William Ruto.

Mwanachama wa vuguvugu la wanawake wa Kanu, Cathy Irungu, jana alisema maajenti hao wamejukumiwa kumvumisha Mwenyekiti wao, Seneta wa Baringo Gideon Moi ili kumweka pazuri kutwaa kiti cha Urais katika uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Usajili wa maajenti hao tayari umeng’oa nanga katika Kaunti za Nyeri, Murang’a, Kiambu, Kirinyaga, Embu, Meru, Tharaka Nithi, Laikipia, Nyandarua na Isiolo huku Bi Irungu akisema lengo lao kuu ni kuhakikisha Dkt Ruto anakosa kushabikiwa na wapigakura wengi wa kaunti hizo.

Bw Moi anatarajiwa kufanya ziara ya kisiasa katika Kaunti ya Nyeri mwezi ujao ambako maajenti 1,560 tayari wamesajiliwa.

Bw Irungu anasisitiza lengo lao sio tu kumzima Naibu Rais ila kuhakikisha Kanu inashinda viti vingi vya ubunge, useneta, uwakilishi wa wadi na ugavana mwaka wa 2022.

Afisa mwengine wa chama hicho naye alifichua kwamba Bw Moi amekuwa akiandaa mikutano ya siri na wazee kutoka kaunti za Mlima Kenya Mashariki (Embu, Meru, Isiolo na Tharaka-Nithi) pamoja na baadhi ya wawakilishi wa wadi.

“Majuma mawili yaliyopita Bw Moi alikutana na kundi la Baraza la wazee wa Njuri Ncheke na baadhi ya madiwani kutoka Meru na Tharaka Nithi katika hoteli ya Fairmount. Pia alikutana na wawakilishi wadi kutoka Bunge la kaunti ya Murangá mwezi uliopita,”

“Lengo letu haswa ni kuhakikisha Dkt Ruto hapati kura nyingi kutoka eneo la Mlima Kenya. Tutamtoa kijasho kwa kuibuka na sera za kuvutia kuhusu kilimo na miundo mbinu zitakazowashawishi wenyeji kutuunga mkono,” akasema afisa huyo ambaye hakutaka jina lake linukuliwe kwa kuwa si msemaji wa chama.

Duru ndani ya chama hicho hata hivyo zinaarifu kwamba gavana wa zamani ambaye haonani uso kwa macho na Dkt Ruto tangu wakosane kuhusu kura za mchujo za Jubilee mwaka wa 2017, ndiye ametwikwa jukumu la kumvumisha Bw Moi akisaidiana na seneta anayehudumu kwa sasa ambaye ni kati ya watu matajiri kutoka Mlima Kenya.

Chama cha Kanu pia kinapanga kuandaa mkutano wa Baraza Kuu la wanachama wake (NDC) mwezi ujao ambako Bw Moi ataidhinishwa kutoka wadhifa wake wa uenyekiti hadi kinara wa chama.

Hii itamweka kwenye kikoa kimoja na viongozi wengine wakuu kama Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Raila Odinga (ODM) na Rais Uhuru Kenyatta (Jubilee).

Bi Irungu ambaye alibwagwa na Rigathi Gachagua katika uchaguzi wa 2017 wa eneobunge la Mathira alisema jamii za Mlima Kenya lazima ziwe na chama mbadala kando na chama cha Jubilee ambacho dalili za kuporomoka kwake zinaendelea kudhihirika kufuatia salamu za maridihiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

You can share this post!

TAHARIRI: EACC ishirikiane na DCI kulinda pesa za wananchi

Matiang’i lawamani kukosa kuzuru eneo la mauaji

adminleo