• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 10:55 AM
Facebook kuzindua mbinu ya kusoma fikra za watu

Facebook kuzindua mbinu ya kusoma fikra za watu

MASHIRIKA Na PETER MBURU

KAMPUNI ya Facebook inatengeneza teknolojia ambayo siku za usoni huenda ikawezesha kusoma fikra za mtu.

Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa kampuni hiyo Mark Zuckerberg alieleza kuwa kampuni hiyo inatafiti mfumo wa kuunganisha akili na kompyuta, alipohojiwa na Profesa Jonathan Zittrain wa Chuo cha Kisheria cha Harvard.

Teknolojia hiyo siku za usoni itawaruhusu watumizi wake kutumia akili tu kuwasiliana na ulimwengu, bila kuandika wanachofikiria wala kufafanua kwa vitendo.

Mfumo huo utawezesha watu kuandika kwa kutumia akili zao ama hata kusongesha vitu kwa kufikiria tu, wawapo katika chumba cha mitambo hiyo.

Watumizi watakuwa wakivaa kifaa kinachofanana na kofia avaayo mtu anapooga kichwani, ambacho kitakuwa na uwezo wa kunakili jinsi damu inazunguka, uchangamfu wa akili na mafikira yenyewe.

Teknolojia hiyo itawezeshwa na hali kuwa hata kwa sasa, watafiti wanaweza kubaini anachofikiria mtu kwa kuangalia namna mishipa ya akili nafanya kazi.

Kifaa cha kusoma akili kitafanya hilo kuwa rahisi zaidi na kwa binadamu kushirikiana na teknolojia, akasema Zuckerberg.

“Jinsi simu zetu zinafanya kazi na mitambo ya tarakilishi, kwa mpango wa apu na kazi zingine si jinsi mpangilio wa akili hufanya kazi ama jinsi tunaiangalia dunia,” Zuckerberg akasema.

“Hii itatupa fursa ya kufanya kazi na teknolojia ambayo inatupa mambo namna tunaifasiri dunia,” akasema.

Hata hivyo, watumizi wa kifaa hicho watakubali kwa hiari yao kabla ya kukitumia, ili kuepuka hali ambapo wanaweza kushtaki kampuni hiyo.

Mnamo 2017, Zuckerberg aliahidi kutoa Sh5 bilioni kuunga mkono kuundwa kwa vifaa vya kuwekwa akilini, kunakili na kuonyesha anachowaza mtu.

Mwaka huo, kampuni ya Facebook ilizindua utafiti wa kiteknolojia ambao ungeruhusu watu kuandika kwenye tarakilishi kwa kufikiria tu.

“Tunaunda mtandao ambapo unaweza kuandika moja kwa moja kutoka akilini kwa kasi ya zaidi ya mara tano ya jinsi unavyoandika kwenye simu yako,” akasema Zuckerberg.

Lakini matamshi hayo ya Zuckerberg yamekuja wakati watumizi wa mtandao wa Facebook wamezidi kupoteza imani na mtandao huo, huku kampuni hiyo ikikumbwa na madai ya kuingilia usiri wa watu.

You can share this post!

Masharti 6 aliyotaka Zidane kabla ya kukubali kuinoa Real...

Arsenal kupumzika Uarabuni wakati wa mechi za kimataifa

adminleo