Kimataifa

Kagame na Museveni wazidi kupakana tope

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

KIGALI, RWANDA

MZOZO wa kidiplomasia kati ya Uganda na Rwanda sasa umefika pabaya , baada ya marais Yoweri Museveni na Paul Kagame kuvamiana kimaneno, katika kile kinachoonekana kama hali inayozidi kutokota.

Wikendi iliyopita viongozi hao, ambao wamekuwa wakilaumiana kuwa wanaingiliana katika masuala ya uendeshaji wan chi zao, walitumia matamshi makali kujibizana, wakati mzozo huo unatishia kufungwa kwa mpaka baina ya mataifa hayo.

Rais Kagame alimlaumu Rais Museveni kuwa amekuwa akiwapa makao wapinzani wake (Kagame), japo Rais Museveni alipinga madai hayo.

“Ninaposikia mtu akisema hakuna yeyote anaweza kutikisa nchi yao, ninakubali. Hakuna yeyote anayefaa kuharibu nchi hiyo, lakini pia nchi hiyo haifai kuharibu nchi zingine,” Kagame akasema alipokuwa akimjibu Museveni.

Matamshi ya Museveni mbeleni yalikuwa kuwa anayejaribu kutikisa taifa lake hangefanikiwa. “Uganda iko imara. Nimesema mbeleni kuwa wanaojaribu kutikisa nchi yetu hawajui uwezo wetu. Ni mkubwa. Tukijikusanya tu hutaweza ikiwa unaleta matatizo,” akasema.

Rais Kagame anasema amechoka kumbembeleza Museveni kuacha kuwahifadhi wapinzani wake. “Unaweza kunipiga risasi ukaniua, lakini kuna kitu kimoja hakiwezekani; hakuna yeyote anaweza kunipigisha magoti.”