• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Si visima vya maji, asema Kagame huku akifunga makanisa 6,000

Si visima vya maji, asema Kagame huku akifunga makanisa 6,000

Na PETER MBURU

RAIS wa Rwanda Paul Kagame mapema Machi alifunga makanisa 6,000 katika taifa lake kufuatia visa vingi vya madai kuwa yanacheza na imani ya raia, na kuamrisha kuwa kila pasta anayetaka kuanzisha kanisa awe na shahada ya masomo ya dini ili kuruhusiwa.

Akiwa katika hafla ya kitaifa eneo la Gabiro, Rwanda Rais Kagame alieleza kughadhabishwa kwake na hali ya kuongezeka kwa makanisa mengi ya kihila, akiuliza ikiwa ni visima vinavyowapa watu maji.

Rais huyo alisema idadi ya maknisa imezidi ile ya viwanda katika nchi hiyo na kuwa hata inahatarisha hali ya usalama.

Bodi ya Uongozi Rwanda aidha ilisema kuwa hatua hiyo inalenga kukaza Kamba katika ufuataji wa sheria za kusajili makanisa nchini humo na kupunguza visa vinavyozidi kuibuka vya viongozi wa kidini ambao wanapora kila peni kutoka kwa masikini kwa njia za kihila.

Baadhi ya raia wa Rwanda tayari wameunga mkono hatua ya Rais wao, wakisema watu wengi wanaanzisha makanisa ili kupata pesa kutoka kwa waumini.

Serikali ya Rwanda ilisema kuwa japo inaheshimu haki za watu kuabudu, kulinda maisha yao ndiyo kazi yake kuu.

Awali mwezi huu, Rais huyo alitangaza kuwa alifunga maelfu ya makanisa na makumi ya misikiti, kama mbinu ya kudhibiti sekta ya dini ambayo serikali imesema mara kwa mara imehatarisha maisha ya waumini.

Akieleza namna alivyoshangazwa na idadi kubwa ya makanisa Jijini Kigali, Rais huyo alisema “Makanisa 700 Kigali pekee? Kwani hivi ni visima ambavyo vinawapa watu maji? Hata sidhani tuna idadi hiyo ya visima. Hata viwanda tuna vingi hivyo kweli? Haya ni makosa.

Alisema kuwa Rwanda haihitaji nyumba nyingi sana za ibada, akisema taifa lake bado ni change kiuchumi.

Hatua yake hata hivyo, imevutia hisia tofauti nchini Rwanda, ambapo wanaharakati wamemkashifu kuwa anakanyaga haki za watu kujieleza. Rais huyo alikana madai hayo.

Wahubiri sita ambao walipinga hatua hiyo walikamatwa na kushtakiwa kwa “kuandaa mikutano haramu kwa lengo baya.”

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Usiseme ‘nimekukosa’ badala yake sema...

Aibu msafishaji kuiba kompyuta ya NMG

adminleo