Habari Mseto

Serikali yatoa Sh2b kukabili njaa, Sh4b bado zahitajika

March 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES LWANGA

WIZARA ya Ugatuzi na Maeneo Kame sasa inataka Sh4 bilioni za kusaidia kupambana na janga la njaa na ukame linaloathiri mamia ya watu katika maeneo kadhaa humu nchini.

Hii ni baada ya serikali Jumatatu kutoa Sh2 bilioni kwa shughuli hiyo, baada ya wizara hiyo kusisitiza kuwa inahitaji Sh6 bilioni kuwakomboa Wakenya kutokana na makali ya njaa na kiu.

Waziri Msaidizi Bw Hussein Dado, alisema tayari wizara imeandiakia hazina ya taifa kuomba fedha hizo ili kusaidia kutatua janga la njaa na ukame unokumba baadhi ya Wakenya.

Akizungumza katika sherehe ya kushinda uchaguzi kwa diwani wa Kipini Magharibi, Bw Musa Wario huko Nduru eneo la Garsen, alisema tayari wameshatayarisha bajeti ya ziada itakayopelekwa bungeni kujadiliwa na kupitishwa ili kusaidia kutatua janga hilo la ukame na njaa.

“Itakapoidhinishwa bungeni, bajeti hiyo itasaidia kupunguza makali ya njaa kwa kununua na kugawa vyakula mbali mbali za kulisha takriban waathiriwa 864,500 katika kaunti 12 nchini,” alisema.

Bw Dado alisema tayari waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa ameanza ziara za kushughulikia janga hilo kwa kutembelea kaunti ya Turkana ambayo imeathirika pakubwa na njaa na ukame.

“Wiki iliyopita, tulitembelea maeneo nane huko Baringo na Turkana ambazo zimeathiriwa na ukame,” alisema na kuongeza “hivi karibuni tutakuja eneo hili la pwani ambapo baadhi ya wakazi katika kaunti ya Kilifi, Kwale ana Tana River wako katika hatari ya kangamizwa na njaa,” alisema.

Katibu Mkuu huyo wa utawala alisema ripoti kutoka baraza la kitaifa la kupambana na ukame (NDMA) inasema kuwa kanti ya Turkana, Mandera, Garissa, Baringo, Kilifi, Tana River, West Pokot, Marsabit, Makueni, Kajiado, Kwale na Isiolo zimeathirika na ukame.

“Katika kaunti ya Kilifi, watu 60,300 katika maeneo ya Ganze, Magarini na Kaloleni wameathiriwa, watu 45,800 katika eneo la Lungalunga na Kinago wameathirika na ukame huko Kwale huku watu 59,700 wakiathiriwa na ukame katika Kaunti ya Tana River eneo la Tana Kaskazini, Mto Tana na mdomo ya Mto Tana,” alisema.

Seneta wa Tana River Juma Wario, diwani wa Bungale Ibrahim Salah ambaye pia ni kiongozi wa wengi bungeni pamoja na madiwani wengine ambao walihudhuria sherehe hiyo waliambia serikali kuu pamoja nay a kaunti zitatue shida ya njaa eneo hilo kwa upesi.

Mnamo Machi mwaka jana kaunti hiyo ilikubwa na janga la mafuriko baada ya Mto Tana kuvunja kingo lake kutokana na mvua kali maeneo ya bara na kuwaacha takriban watu 100,000 bila makazi.

Kwengineko, mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu (KRCS) katika Kaunti ya Kilifi, Bi Hakima Masoud alisema wamejitahadhari kutokana na janga hilo huo kuzuia vifo.

“Tayari tunafuatilia patani ya mvua ambayo inatarajiwa kuanza mwezi Machi na Aprili,” alisema na kuongeza “baadhi ya bwawa za maji katika eneo la Magarini na Ganze zimeanza kukauka na ukame huenda ikaongezeka endapo mvua itachelewa kunyesha.”